Kiswahili katika miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara

December 9, 2021 7:25 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Chatumika kuwaunganisha Watanzania.
  • Ni lugha rasmi katika jumuiya za kimataifa.
  • Lugha muhimu ya kufanyia biashara Afrika.

Dar es Salaam. Licha ya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa la Tanzania, lakini sasa imepiga hatua kubwa hadi kuwa chombo muhimu cha mawasiliano kinachounganisha jumuiya za kimataifa na shughuli za biashara.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru leo Disemba 9, 2021 amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika lugha ya Kiswahili.

“Nchi nyingi zinatumia lugha za kigeni kama lugha za mataifa yao zinazowaunganisha, inapendeza kuona kuwa tunatimiza miaka 60 tukiwa wamoja wenye utambulisho mmoja na lugha moja ya Kiswahili inayoendelea kupata umaarufu kimataifa   siku hadi siku” amesema Rais Samia wakati akilihutubia Taifa jana.

Wakati Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, Kiswahili haikuwa lugha inayozungumzwa na watu wote ndani ya Tanganyika bali kizazi kilichofuata baada ya uhuru walijifunza kiswahili shuleni. 

Hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa kati ya nchi chache zenye lugha ya Taifa yenye asili ya nchi husika. 

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema kuwa katika miaka 60 ya uhuru, Tanzania imefanikiwa kushawishi Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi zinazotumika  katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini  mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU).


Soma zaidi: 


Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa Sayansi na Elimu (UNESCO) limepitisha azimio la kutenga siku ya Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Azimio hilo linaifanya lugha ya Kiswahili kuwa ya kwanza katika bara la Afrika kutambuliwa na kutengewa siku yake rasmi na UN.

Akiongea na Waandishi wa Habari hivi karibuni, mara baada ya UNESCO kupitisha rasmi azimio hilo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa aliwataka wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini kuendelea kutumia lugha hiyo ili iendelee kukua duniani.

Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa Kiswahili ni lugha ya biashara ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kuwafaidisha wafanyabiashara.

Ripoti ya utafiti wa masuala ya kifedha ya Finscope ya mwaka 2017 inabainisha kuwa watu saba kati 10 (asilimia 72) nchini wanaweza kusoma na kuandika Kiswahili vyema ikilinganishwa na takriban watatu tu kwa kila 10 wanaoweza kufanya hivyo katika Kiingereza.

Licha ya Kiswahili kuwa lugha ya biashara, bado wafanyabiashara watatakiwa kutumia lugha zingine kuvutia wateja wengi zaidi ikizingatiwa kuwa utafiti huo unaeleza kuwa robo ya Watanzania au asilimia 25 hawawezi kusoma wala kuandika Kiswahili.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW