Mgonjwa mwingine wa Corona afariki dunia Tanzania, wagonjwa wafikia 147
- Kufariki kwa mgonjwa huyo, kunaifanya Tanzania hadi sasa kupoteza watu watano mpaka sasa.
- Wagonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) Tanzania wameongezeka na kufikia 147 baada ya Serikali kutangaza wagonjwa wapya 53.
- Jiji la Dar es Salaam ndiyo kitovu cha ugonjwa huo baada ya kuwa na wagonjwa 100.
Dar es Salaam. Wakati wagonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) Tanzania wakizidi kuongezeka na kufikia 147 baada ya Serikali kutangaza wagonjwa wapya 53, Wizara ya Afya imesema mgonjwa mmoja aliyekuwa akiugua ugonjwa huo amefariki dunia.
Kufariki kwa mgonjwa huyo, kunaifanya Tanzania kupoteza watu watano mpaka sasa kutokana na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema jana na leo walipeleka sampuli za wagonjwa katika maabara ya Taifa na vipimo vimeonyesha kuwepo kwa watu 53 wapya wenye virusi vya Corona.
Kiwango hicho cha wagonjwa waliobanika leo ni cha juu kuwahi kuripotiwa kwa siku moja tangu Aprili 15 ambapo Wizara ilithibitisha visa 29.
Ndani ya siku tatu idadi ya wagonjwa wa COVID-19 Tanzania imeongezeka zaidi ya mara moja kutoka wale waliokuwepo Jumanne wiki hii.
Ummy amesema kuwa kati ya wagonjwa hao wapya, 38 wapo Dar es Salaam, 10 wapo Zanzibar, Kilimanjaro (1), Mwanza (1), Lindi (1), Kagera (1) na Pwani mmoja.
“Wagonjwa hawa wote ni Watanzania,” amesema Ummy wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ugonjwa huo jijini Dar es Salaam leo (Aprili 17, 2020).
Idadi ya wagonjwa hao wapya inafanya Dar es Salaam kuendelea kuwa kitovu cha COVID-19 baada ya kuwa na wagonjwa 100 kati ya 147 waliopo nchini.
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Kwa mara ya kwanza ugonjwa huo pia umepiga hodi katika mikoa miwili ya Lindi na Pwani baada ya kila mmoja kuripoti mgonjwa wa kwanza.
Hii ina maana kuwa kwa sasa COVID-19 imeshaingia kwenye mikoa saba ya Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.
“Hivyo sasa, jumla ya watu waliopata maambukizi ya COVID-19 nchini tangu tulipotangaza mgonjwa wa kwanza Machi 16, 2020 ni 147. Watu waliopona ni 11, waliofariki watano, wagonjwa wote waliobaki (131) hali zao ni nzuri isipokuwa wagonjwa wanne ambao wanapatiwa matibabu ya wagonjwa mahututi kutokana na kusumbuliwa na matatizo mengine ya kiafya,” amesema Ummy.
Mwalimu amesema Serikali inaendelea kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kama wanavyopatiwa taarifa na elimu mara kwa mara.
Tahadhari hiyo ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kutokugusa macho, pua na mdomo.
Aidha, Ummy ameitaka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuacha kupokea wagonjwa wenye dalili za Corona na ijielekeze kushughulikia rufaa za magonjwa mengine kwa sababu ndiyo hospitali kuu ya rufaa ya kitaifa bali waende katika vituo vilivyoainishwa ikiwemo hospitali ya rufa ya mkoa ya Amana ya jijini Dar es Salaam.
Latest
