Mgao wa maji: Majaliwa akagua visima vya dharura Dar
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Oktoba 10, 2022 amekagua visima vya dharura vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa katika mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi na kuagiza zoezi hilo pamoja na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali liwe endelevu. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Ataka zoezi la uchimbaji na utunzaji wa visima uwe endelevu.
- Visima 160 kupunguza makali ya mgao wa maji jijini hapa.
- Mahitaji ya maji ni lita milioni 540 lakini kwa sasa uzalishaji ni lita milioni 300.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua visima vya dharura vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa katika mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuagiza zoezi hilo pamoja na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali liwe endelevu.
Ukaguzi huo umekuja wakati wananchi wa mkoa huo unaokuwa kasi wakiwa katika mgao wa maji na umeme kutokana na kupungua kwa maji katika Mto Ruvu kulikochangiwa na kuchelewa kwa mvua za vuli.
Hali hiyo imesababisha usumbufu kwa wakazi hao huku katika baadhi ya maeneo maji yakikosekana kwa zaidi ya wiki tatu mfululizo.
Majaliwa amekagua visima katika eneo la Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma leo Novemba 10, 2022 ambapo ameshuhudia usafishwaji wa visima hivyo pamoja na zoezi la usambazaji maji.
Visima hivyo ni miongozi mwa visima 197 vilivyochimbwa na Serikali mkoani Dar es Salaam ambapo kwa sasa 160 vimefufuliwa na kutoa lita milioni 29.4 kwa siku.
Maji hayo yameunganishwa katika mfumo ili kusaidia kupunguza changamoto ya maji.
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Bonde la Wami Ruvu pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) waendelee kufanya tafiti kubaini maeneo yenye maji mengi na kuchimba visima na kuyaingiza katika mfumo.
Amewataka wananchi kuendelea kulinda maeneo yote yenye vyanzo vya maji pamoja na kuyatumia vizuri maji yanayopatikana ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji hususani katika kipindi hiki cha ukame.
Soma zaidi:
Aidha, amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mikoa yote nchini likiwemo jiji la Dar es Salaam kwa kutekeleza kampeni mbalimbali ikiwemo ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi.
Mahitaji ya maji katika mkoa huo uliopo katika mwambao wa bahari ya Hindi ni lita milioni 544 kwa siku na uzalishaji maji kwa siku ni lita milioni 520 katika kipindi ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kinakuwa katika hali ya kawaida.
Hata hivyo, katika kipindi hiki ambacho kiwango cha maji kimepungua katika Mto Ruvu uzalishaji wa maji nao umepungua na kufikia lita milioni 300 kwa siku.
Baada ya kuingiza lita milioni 70 kutoka katika mradi wa visima vya wilayani Kigamboni na lita milioni 29.4 kutoka katika mradi wa visima vingine 160 vya jijini Dar es Salaam sasa upungufu wa maji ni lita milioni 145 kwa siku.
Takribani asilimia 40 ya eneo la mkoa halina mtandao wa mabomba ya DAWASA kutokana na uwekezaji mdogo, hivyo kulazimika kutumia visima kama vyanzo vikuu vya huduma ya maji.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini wizara yake imejipanga kuchimba mabwawa kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua na kuyaingiza katika mfumo.
“Tutashinda site kuhakikisha maji yanapatikana kwa wananchi,” amesema Aweso.