Ni shida: Wapasua mwamba kupata maji
- Ni wananchi wa vijiji vya Kanyerere na Fella mkoani Mwanza.
- Wafanya hivyo baada ya visima na malambo kukauka.
- Kuchelewa kwa mvua kwachangia.
Mwanza. Ni asubuhi na mapema, wakazi katika vijiji vya Kanyerere na Fella wilayani Misungwi wanakusanyika kwenye mwamba kuteka maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kunyweshea mifugo.
Licha ya kuwa vijiji vyao kuwa kilomita 30 kutoka katikati ya jiji la Mwanza ambako ndipo kilipo chanzo cha maji cha Kapripoint, lakini ukosefu wa maji unawalazimu kuamka usiku wa manane angalau wapate hata ndoo mbili za kutumia.
Wapo baadhi ya wakazi ambao wanalazimika kuchimba mashimo chini ya miamba ili kutafuta maji ya kutumia kutokana na uhaba wa maji unaoendelea kutikisa katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo wa Kanda ya Ziwa.
Wapo baadhi ya wakazi ambao wanalazimika kuchimba mashimo chini ya miamba ili kutafuta maji ya kutumia kutokana na uhaba wa maji unaoendelea kutikisa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mwanza.
Kuchelewa kwa mvua za masika kumechangia hali ya ukosefu wa maji kwenye maeneo hayo.
Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imetembelea Kanyerere na Fella na kuzungumza na wananchi ambao walieleza ukosefu wa maji katika kipindi hiki ni mkubwa na haujawahi kutokea miaka mingi sasa.
Adelina Masanja ni mkazi wa Kijiji cha Fella wilayani Misungwi anasema wao hawana mabomba ya maji na kuwa katika miaka yote wanatumia maji ya visima na kwenye malambo.
“Kipindi hiki kumekuwepo na mabadiliko makubwa hasa baada ya mvua kuchelewa, visima vyote vimekauka na tumebakiwa na kisima kimoja tu ambacho tunalazimika kuamka alfajiri kwenda kuchota na kisha baadaye yanakauka hadi kusubirisha tena,” anasema Adelina.
Kisima kilichochimbwa kwa ajili ya kupata maji ya kutumia katika kijiji cha Fella mkoani Mwanza. Kisima hicho kilikauka na hakijafukiwa. Picha | Mariam John.
Hofu kubwa waliyonayo wakazi hao ni wafugaji ambao wana mifugo mingi ambapo licha ya kuwa wanachimba visima ili kupata maji ya kunywesha mifugo yao lakini bado visima hivyo vinakauka.
“Tunamuomba Mungu alete mvua ili kunusuru mifugo yetu, bado hatujapata tatizo la mifugo kufa kwa kukosa malisho na maji, lakini hali ikiendelea hivi hali itakuwa mbaya si kwenye mifugo pekee bali hata kwa binadamu,” anasema Manota Shiriwa, mkazi wa Kijiji cha Fella.
Shiriwa ambaye anamiliki ng’ombe 15 na mbuzi 20 anasema anapitia wakati mgumu kwani kwa siku analazimika kuwa angalau na mapipa matatu ya maji kwa ajili ya mifugo yake na kuwa anachokifanya hivi sasa ni kuinywesha mara moja pekee.
Septemba mwaka huu alichimba kisima na alipata maji lakini hayakukawia kukauka kutokana na kuwepo kwa jua na upepo mkali ambao unakausha maji haraka.
“Tunatamani tungekuwa na maji ya bomba tungepunguza changamoto kama hizi ambazo zinatulazimu kutembea umbali mrefu wa takribani masaa mawili kufuata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kunyweshea mifugo kwa kweli hali ni mbaya,” anasema Shiriwa.
Soma zaidi:
- Nusu ya wanafamilia walivyokatwa miguu kwa “ugonjwa wa ajabu”- 1
- Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi
- Simulizi ya familia, nyumba zilizozingilwa na maji ya Ziwa Victoria
Kasi ya uharibifu wa mazingira
Licha ya kwamba wakazi katika Kijiji hicho hupasua miamba kwa ajili ya kupata maji, lakini Nukta habari ilishuhudia kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na uchimbaji wa visima holela.
Visima vingi vilivyochimbwa na kukauka maji vimeachwa na wananchi hawajachukua jukumu la kufukia mashimo hayo ambayo yanaweza kusababisha athari kwa siku za baadae pale mvua zitakapoanza kunyesha.
Pia katika vijiji hivyo viwili, kuna kasi kubwa ya ukataji miti hali inayosababisha maeneo mengi kuwa jangwa ambapo baada ya kuzungumza na wakazi wa maeneo hayo walisema wanakata miti kwa ajili ya kuni na mkaa wa kupikia.
“Ni kweli mashimo hayafukiwi yanaachwa hivyo ili mvua ikija maji yajae kwa ajili ya matumizi ya baadae na ndio maana hawachukui jukumu la kufukia,” anasema Thabiza Hoja.
Kuhusu suala la ukataji wa miti, Thabiza anasema ni kwa ajili ya kuni “hatuna uwezo wa kununua gesi za kupikia ndiyo maana tunatumia nishati ya kuni,”
Tangazo:
Hatua zinazochukuliwa
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kanyerere, Mathias Inogu amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya ukosefu wa maji na kueleza kuwa Serikali inafanyia kazi ili kusogezea wananchi huduma ya maji karibuni na nyumbani.
Anasema kinachofanyika hivi sasa ni wananchi kwenda kufuata maji kwenye huo mwamba ambapo pia kuna wakati yanakatika hivyo kusubiria kwa muda kisha wachote tena.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Mwanza, Godfrey Sanga anasema Ruwasa inatekeleza jumla ya miradi 544 ya maji katika maeneo mbalimbali ya vijiji vya mkoa wa Mwanza.
Anasema miongoni mwa miradi hiyo upo wa Kigongo ambako kunajengwa chanzo cha maji kitakachosambaza maji katika vijiji vya Identemya, Usagara, Fella na Ukirigulu. Ujenzi wa chanzo hicho kwa sasa kimefikia asilimia 60 na kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
“Tunayo miradi mingi, mingine ipo kwenye usanifu na mingine ipo kwenye hatua za ukamilishaji, tunakusudia kupunguza tatizo la maji kwenye maeneo ya vijijini kwa asilimia 85 ifikapo 2025, hivyo wananchi wawe na subira kidogo,” anasema Injinia Sanga.
Sanga anasema Ruwasa imepanga kutumia zaidi ya Sh88 bilioni kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji vijijini ifikapo 2025.
Pamoja na nia njema ya Serikali kupunguza changamoto za maji vijijini anasema baadhi ya wananchi wanaihujumu miundombinu hali inayosababisha kurudisha nyuma utendaji kazi.