Rais Samia ataja sababu 4 mgao, uhaba wa maji Dar
Rais samia aliyekuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliofanyika leo Novemba Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam amesema kupungua kwa maji katika mto Ruvu kunasababishwa na ukataji wa miti hususani mkoani Pwani. Picha | Ikulu.
- Ukataji wa miti watajwa kama chanzo kikuu cha uhaba wa maji Dar.
- Makala asema lita milioni 70 za maji zinaingia usiku leo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu mbalimbali zinazochangia jiji la Dar es Salaam kupata changamoto ya uhaba na mgao wa maji ikiwemo mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za binandamu.
Rais samia aliyekuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliofanyika leo Novemba Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam amesema kupungua kwa maji katika mto Ruvu kunasababishwa na ukataji wa miti hususani mkoani Pwani.
“Na katika mikoa inayoongoza kwa wingi wa ukataji wa misitu kwa ajili ya mkaa ni Mkoa wa Pwani uliopo kwenye mto Ruvu unaopunguza flow (mtiririko) wa maji kwenye mitambo inayoleta maji Dar es Salaam,” amesema Rais Samia.
Mto Ruvu umekuwa ni chanzo muhimu cha maji kwa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini inayozalisha bidhaa hiyo inayotumika zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Sababu nyingine aliyotaja Rais Samia ni tabia za baadhi ya wananchi kuziba njia za maji zinazoleta maji Dar es Salaam.
“Na yale yanayokwenda unakuta wale wanaolima wamezuia njiani …watu wamejenga mabwawa wanafuga na samaki humo humo,” amesema Rais.
Akihutubia washiriki wa mjadala huo katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Rais Samia ameitaja changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya maji iliyopo jijini hapa ambayo haiendani na idadi ya watu nayo huchangia uhaba wa maji.
“Pengine miundombinu mingine ilijengwa huko Dar es salaam ikiwa na watu milioni 3 na sasa hivi ni milioni 5, wale mnaohusika na maji muangalie maunganisho wa maji ndani ya jiji la Dar es Salaam,” amesisitiza Rais.
Soma zaidi:
Mpangilio wa makazi uliopo jijini humo umetajwa pia na Rais Samia kama moja ya changamoto inayosababisha miundombinu bora ya maji isifike kwenye baadhi ya maeneo jijini humo.
Kauli hiyo ya Rais Samia ni imekuja baada ya kuibuka kwa mjadala kuhusu mgao wa maji jijini humo uliodumu kwa zaidi ya wiki mbili huku maeneo mengine yakikosa kabisa huduma hiyo.
Baadhi ya wadau wakiwemo watumiaji wa mitandao ya kijamii, wameshauri Serikali kuongeza vyanzo vingine vya kuzalisha maji na kutokutegemea moja kwa moja Mto Ruvu.
Mkutano huo wa nishati ya kupikia unafanyika kwa siku mbili ukihusisha wadau kutoka sekta mbalimbali nchini kutafuta suluhu ya changamoto zinazoletwa na nishati chafu za kupikia.
Suluhu yapatikana
Awali mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala amesema changamoto ya maji jijini Dar es Salaam imeshatatuliwa na wananchi wataanza kupata maji kuanzia leo usiku.
“Ili kupunguza ukali wa maji ya mgao jijini Dar es Salaam nina furaha kuripoti kwako kuwa leo usiku tunaingiza maji kutoka Kigamboni katika visima 12…lita milioni 70 zitaingia mjini,” amesema Makala.
Latest
