Uvunaji wa maji ya mvua kumaliza tatizo la mgao Dar?

November 15, 2022 12:02 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia kuangaza kutekeleza mpango wa uvunaji maji.
  • Bwawa kubwa kujengwa Kigamboni kuhifadhi maji hayo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaanza utekelezaji wa uchimbaji wa mabwawa na uvunaji wa maji ya mvua ili kupunguza uhaba wa maji unaojitokeza kipindi cha kiangazi hasa jijini Dar es Salaam. 

Rais Samia aliyekuwa akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa maji, ugawaji wa mitambo ya kuchimba visima na mabwawa na makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, iliyofanyika leo Novemba 11, 2022, Kigamboni, Jijini Dar es Salaam amesema uvunaji huo utapunguza upotevu wa maji ya mvua yanayoishia baharini

“Mvua zinaponyesha  Tanzania inapoteza  mamilioni ya lita za maji baharini, tunalia na kuongezeka kwa kina cha bahari lakini tunayaachia maji  yanakwenda,” amesema Rais.

Akihutubia wananchi na viongozi mbalimbali kwenye Wilaya hiyo Rais Samia  ameeleza namna mradi huo wa ukusanyaji wa maji ya mvua ulivyoshindikana miaka ya nyuma na kuwaomba baadhi ya wajumbe wa kamati iliyokuwepo kipindi hicho kushirikiana kuufufua.

“Tulifanya kazi kubwa lakini haikutekelezwa, tulitoa mapendekezo mengi lakini hayakutekelezwa…naomba mkanisadie yaende yakatelezeke” amesema Rais Samia bila kuitaja kamati hiyo. 

Utekelezaji wa mradi huo huenda ukapunguza uhaba na mgao wa maji nchini  hususani jiji la Dar es Salaam ambao unatokana na ukame uliosababishwa na kuchelewa kwa mvua za vuli ambao huanza kunyesha Oktoba.

Mradi wa bwawa la Kidunda uliokabishiwa leo kwa mkandarasi ndilo litatumika kwenye uvunaji wa maji ya mvua utakaofanyika nchini.

Bwawa hilo linalojengwa kwa gharama ya Sh329 bilioni likikamilika litahakikisha upatikanaji wa maji kwenye jiji la Dar es Salaam kwa miaka mitatu mfululizo.

“Bwawa hili sio la leo na kesho ni bwawa litakalochukua miezi 30 lakini ujazo wake utategemea jinsi mvua zitakapokuja…bwawa likijaa tunategemea kutokuwa na shida ya maji kwa Dar es Salaam na viunga vyake,” amesisitiza Rais.

Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuwasha mtambo (pampu) wa kusukuma maji kwenye tanki kubwa la maji kwa ajili ya usambazaji kwa wakazi wa maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Novemba, 2022. Picha | Ikulu.

Lindeni vyanzo vya maji mto Ruvu 

Rais Samia amewataka viongozi wa Serikali hususani wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kulinda chanzo cha maji cha mto Ruvu kwani ndio suluhisho pekee la uhaba wa maji kwenye mkoa huo.

“Niwaombe sana tufanye kazi wote kwa pamoja wakuu wa mikoa wakuu wa wilaya tufanye kazi kwa pamoja kutunza vyanzo vya maji,” amesema Rais.

Aidha, Rais Samia amesikitishwa na vitendo vya baadhi vitendo vya uharibifu wa mto Ruvu vinavyofanywa na wananchi na kuagiza Wizara ya Maji kutafuta suluhu ya vitendo hivyo.

“Inashangaza kuona wananchi wamerudia mambo yale yale hivyo nawaagiza mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na mkuu wa mkoa wa Pwani kuangalia namna mtakavyofanya kukomesha vitendo hivyo,” ametoa agizo hilo Rais.

Sambamba na hilo amesisitiza wakandarasi wa mradi wa Kigamboni aliouzindua leo pamoja na mkandarasi wa mradi wa bwawa la Kidunda kufanya kazi kwa  bidii na kukamilisha kwa wakati.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW