Mfumuko wa bei wazidi kupaa Tanzania
- Umepanda hadi kufikia asilimia 4.2 kwa mwaka ulioishia Desembe 2021 kutoka asilimia 4.1 iliyorekodiwa Novemba 2021.
- Hiyo ni baada ya kuongezeka kwa bei za baadhi ya vyakula na zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma Tanzania imepanda hadi kufikia asilimia 4.2 kwa mwaka ulioishia Desembe 2021 kutoka asilimia 4.1 iliyorekodiwa Novemba 2021, ikichagizwa zaidi na kuongezeka kwa bei za baadhi ya vyakula na zisizo za vyakula.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishi Desemba 2021 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo mwaka ulioishia mwezi Novemba 2021.
“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2021 umeongezeka kidogo hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2021.
“Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Desemba 2021 umepungua hadi asilimia 3.9 kutoka asilimia 4.0 ilivyokuwa mwezi Novemba, 2021.” inasomeka sehemu ya ripoti ya mfumuko wa bei ya NBS iliyotolewa leo (January 10, 2022).
Zinazohusiana:
NBS imesema kuwa baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupanda kwa kasi ya bei kwa mwezi Desemba ni pamoja na mchele kwa asilimia 3.7, mahindi (asilimia 5.2), unga wa ngano (asilimia 3.4), unga wa mahindi kwa (asilimia 3.3) na nyama ya ng’ombe kwa asilimia 2.3.
Pia nyama ya mbuzi imepanda kwa asilimia 1.6, samaki (asilimia 5.3), matunda (asilimia 3.7), mbogamboga (asilimia 2.3) na viazi kwa asilimia 3.2.
Bidhaa nyingine zisizo za vyakula ambazo kasi ya mfumuko wa bei imepanda ni vifaa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za makazi kwa asilimia 5.0, gesi (asilimia 2.3), mafuta ya taa (asilimia 1.7), dizeli (asilimia 6.7) na petroli kwa asilimia 3.0.

Bidhaa za vyakula hutumika zaidi katika kaya za Tanzania kutokana na umuhimu wake kwenye maisha ya kila siku na pia ni chanzo cha kipato kwa familia zinazojishughulisha na kilimo cha mazao na uzalishaji viwandani.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa mfumuko wa bei kupanda baada ya kuduma kwa miezi miwili katika robo ya nne ya mwaka 2021.
Kasi ya mfumuko wa bei wa Taifa katika mwaka ulioshia Novemba 2021 ilikuwa asilimia 4.1 kutoka asilimia 4 iliyorekodiwa Oktoba 2021 baada ya kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo.
Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba 2021 ilikuwa asilimia 4 sawa kabisa na ilivyokuwa Septemba mwaka huu jambo lililoonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.
Latest