Mfumuko wa bei wapaa baada ya kudumaa kwa miezi miwili mfululizo

December 8, 2021 12:56 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Umeongezeka hadi asilimia 4.1 kutoka asilimia 4.
  • Umechangiwa na kupanda kwa baadhi ya bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei wa Taifa imeongezeka kidogo katika mwaka ulioshia Novemba 2021 hadi asilimia 4.1 kutoka asilimia 4 iliyorekodiwa Oktoba 2021 baada ya kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo.

Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba 2021 ilikuwa asilimia 4 sawa kabisa na ilivyokuwa Septemba mwaka huu jambo lililoonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.

Kupanda kwa kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Novemba kumechangiwa na kupanda kwa baadhi ya bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika taarifa ya mfumuko wa bei iliyotolewa na leo Desemba 8, 2021 imeeleza kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba, 2021 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Oktoba 2021.

“Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioshia mwezi Novemba 2021 kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula,” imeeleza NBS katika taarifa yake..

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na unga wa ngano kwa asilimia 8, nyama ya ngombe (asilimia 4.3), maziwa ya unga (asilimia 3.4) na mayai kwa asilimia 49.

Bidhaa zingine ni viazi vitamu kwa 2, asali (asilimia 4.0) na viungo vya kupikia kwa asilimia 3.5.


Soma zaidi


Mbali na bidhaa za vyakula, kupanda kwa mfumuko wa bei pia kumesababishwa na bidhaa zisizo za vyakula ikiwemo vinywaji vyenye kileo na mavazi.

Huduma ya malazi kwenye mahoteli na nyumba za kulala wageni zimepanda kwa asilimia 6.5, vinywaji vyenye kileo (asilimia 2.7), mavazi (asilimia 5.4), kodi ya pango (asilimia 5.3) na gesi ya kupikia kwa asilimia 3.2.

Bidhaa zingine ni mkaa ambao umepanda hadi asilimia 1.8, majokofu (asilimia 4.3), vyombo vya nyumbani (asilimia 8.8), simu za kiganjani (asilimia 3.4) na runinga kwa asilimia 3.5.

“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Novemba, 2021 umeongezeka hadi asilimia 4.4 kutoka asilimia 3.9 mwaka ulioishia Oktoba mwaka huu,” imeandika NBS.

Pamoja na hayo, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Novemba, 2021 umepungua kidogo hadi asilimia 4 kutoka asilimia 4.1 ilivyokuwa Oktoba, 2021.

Ahueni, hali tete kwa majirani 

Wakati mfumuko wa bei ukipanda Tanzania, kwa majirani zetu hali ni tete na ahueni. Mathalan, Kenya huenda wakazi wa nchi hiyo wakawa na kicheko baada ya mfumuko wa bei kupungua hadi asilimia 5.80 kutoka asilimia 6.45 kwa mwaka ulioishia Oktoba 2021.

Uganda, mfumuko wa bei umeongezeka hadi asilimia 2.6 kutoka asilimia 1.9 kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2021.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW