Mfumuko wa bei washuka Tanzania baada ya ‘kuganda’ kwa miezi miwili
- Washuka baada ya kung’ang’ania katika kiwango cha asilimia 3.7 kwa miezi miwili mfululizo.
- Umeshuka hadi asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Machi 2020 kutoka asilimia 3.7 iliyorekodiwa Februari mwaka huu.
- Umechagizwa na kupungua kwa gharama za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeshuka hadi kufikia asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Machi 2020 kutoka asilimia 3.7 iliyorekodiwa Februari mwaka huu, ikichagizwa na kupungua kwa gharama za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Machi 2020 kumekuja baada ya kasi yake kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo.
Mwezi uliopita NBS ilieleza kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Februari 2020 ulikuwa asilimia 3.7 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Januari 2020.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Zinazohusiana: Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Januari
Ripoti ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa Aprili 8, 2020, imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula ikilinganishwa na Februari mwaka huu.
Mfumko wa bei wa bidhaa zisizo za chakula ambazo umeshuka ni pamoja na majiko ya gesi ambayo imeshuka kwa asilimia 2.3, viyoyozi kwa asilimia 1.1, mafuta ya nywele (asilimia 2.7) na bidhaa binafsi za mapambo kama saa kwa asilimia 2.9.
Kwa upande wa bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 5.3 kutoka asilimia 5.9 kama ilivyorekodiwa Februari 2020.
