Ahueni mfumuko wa bei ukishukaTanzania

July 10, 2023 1:08 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Umeshuka hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Juni 2023 kutoka asilimia 4.0 iliyorekodiwa Mei mwaka huu.
  • Umechagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeendelea kushuka kwa miezi mitatu mfululizo hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Juni 2023 ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Mfumuko wa bei wa Juni umeshuka kutoka asilimia 4 iliyorekodiwa Mei mwaka huu ambapo pia ulishuka kutoka asilimia 4.3 ya mwaka ulioishia Aprili 2023. 

Taarifa ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo Julai 10, 2023 imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na zisizokuwa za chakula mwezi Juni, 2023 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Mei, 2023.

Kiwango cha juu zaidi cha mfumuko wa bei kuwahi kuripotiwa tangu Mei 2022 ni kile kilichorekodiwa Oktoba na Novemba 2022 na Januari mwaka huu cha asilimia 4.9.


Soma zaidi


Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Juni 2023 ni mchele kutoka asilimia 23.8 hadi asilimia 17, unga wa ngano (kutoka asilimia 2.8 hadi asilimia 1.8), unga wa mahindi (kutoka asilimia 45.6 hadi asilimia 30.5) pamoja na maharage kutoka asilimia 29.7 hadi asilimia 28.6. 

Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na vifaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa nyumba kutoka asilimia 4.4 hadi asilimia 0.6, nishati ya gesi (kutoka asilimia 7.3 hadi asilimia 0.9) na mafuta ya taa kutoka asilimia -2.5 hadi asilimia -8.8. 

“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2023 umepungua hadi asilimia 7.8 kutoka asilimia 8.5 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2023,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Juni 2023 nao umepungua hadi asilimia 1.8 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2023.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW