Mfumuko wa bei wang’ang’ania pale pale miezi miwili mfululizo
- Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Julai 2019 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.7 kama ilivyokuwa Juni.
- Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai 2019 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 2.9 kutoka asilimia 2.3 ilivyokuwa Juni 2019.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Julai 2019 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa Juni mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Julai 2019 ulikuwa asilimia 3.7 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Juni 2019.
Akizungumza leo (Agosti 9, 2019) jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka NBS, Ruth Minja amesema hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi za vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kilichoishia Julai 2019.
Zinazohusiana: Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Januari
Aidha, Minja amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai 2019 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 2.9 kutoka asilimia 2.3 ilivyokuwa Juni 2019.
“Baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi Julai zikilinganishwa na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia sita, unga wa mhogo (asilimia 4), mafuta ya kupikia (asilimia 8.9), na mbogamboga (asilimia 4.6).
“Kwa upande wa bidhaa zisizokuwa za vyakula ni pamoja na vifaa vya kieletroniki, majiko ya gesi pamoja na vifaa na bidhaa za huduma,” amesema Minja.
Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, amesema taarifa inaonyesha kuwa Kenya ilikuwa na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei Julai 2019, ambapo kiwango chake kilifikia asilimia 6.27 ikilinganishwa na asilimia 5.70 kwa mwaka ulioishia Juni 2019.
Taarifa ya mfumuko wa bei katika nchi ya Uganda katika mwaka ulioishia Julai 2019, zinaonyesha kuwa nchi hiyo ilikuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa mdogo bei kilichofikia asilimia 2.6 kutoka asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Juni, 2019.