Mfumuko wa bei Tanzania wanasa kiwango cha Aprili 2025
- Kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa za vyakula.
- Mfumuko wa bei wapungua Kenya, waongezeka Uganda.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Mei 2025 umeng’ang’ania katika kiwango cha asilimia 3.2 kama ilivyoripotiwa Aprili, 2025 ikichangiwa zaidi na kupungua kwa kasi ya bei za bidhaa zisizo za vyakula.
Mfumuko wa bei ni kasi ya ongezeko la bei ya bidhaa na huduma nchini na kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa kusalia kwa kasi hiyo ya mfumuko wa bei kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa za vyakula.
Tangu Januari mwaka huu mfumuko wa bei umekuwa ndani ya wigo wa malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan wa asilimia 5 baada ya kuwa kati ya asilimia 3.1 na . Kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kurekodiwa mwaka huu ni asilimia 3.3 kilichorekodiwa Machi, 2025.
Taarifa ya NBS iliyotolewa leo Juni 9, 2025 imeeleza kuwa baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na ulezi kutoka asilimia 38.0 hadi asilimia 43.0 na unga wa mahindi kutoka asilimia 2.3 hadi asilimia 9.8.
Mbali na bidhaa hizo, ofisi hiyo imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa mikate na vyakula vingine vya kuoka mfano maandazi vitumbua na chapati nao uliongezeka kutoka asilimia 16.6 hadi asilimia 17.3 wakati mtama ukifikia asilimia 2.3 kutoka asilimia 2.1 iliyorekodiwa Aprili, 2025.
Kuongezeka kwa bei ya nyama ng’ombe ambayo ni moja ya kitoweo mashuhuri nchini, NBS imesema kulifanya mfumuko wa bei wa bidhaa hiyo kuongezeka kutoka asilimia 18.9 hadi asilimia 19.8.
“Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na viatu vya wanaume kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 2.2…na bidhaa muhimu za nyumbani kama majokofu, na majiko ya kupikia (kutoka asilimia 3.2 hadi asilimia 2.7,” imeeleza taarifa hiyo ya NBS.

Hata hivyo, NBS imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2025 umeongezeka hadi asilimia 5.6 kutoka asilimia 5.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2025.
“Mfumuko wa Bei usiojumuisha bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Mei, 2025 umepungua hadi asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2025,” imesema taarifa ya NBS.
Maumivu Uganda, ahueni Kenya
Wakati mfumuko wa bei uking’ang’ania katika kiwango kile kile Tanzania, NBS imeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa nchi jirani ya Kenya umepungua hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2025.
Nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei 2025 umeongezeka hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 3.5 kwa mwaka ulioishia Aprili 2025.
Latest



