Mfumuko wa bei waongezeka Tanzania

September 10, 2024 5:45 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Waongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3 iliyokuwepo Julai.
  • Ni kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za chakula.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini kwa mwaka unaoishia Agosti 2024 imeongezeka kiduchu hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.0 ukichangiwa zaidi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula.

Hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2024.

Ongezeko hilo ni la nne kurekodiwa ndani ya kipindi cha miezi saba iliyopita ambapo ndio kiwango kikubwa zaidi kwa mwaka 2024 ingawa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai kilishuka hadi asilimia 3.0.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo Septemba 10, 2024 imebainisha kuwa kuongezeka kwa kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti 2024 kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za chakula.

“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024 umeongezeka hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 1.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024,” imebainisha taarifa ya NBS.

Tangu mwaka 2024 uanze kasi ya mfumuko wa bei imekuwa kati ya asilimia 3.0 na 3.1, kiwango ambacho kipo ndani ya wigo wa Serikali wa kuwa na mfumuko wa bei kati ya asilimia 3.0 na asilimia 5.0. 

Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za yvakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024 umepungua hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024.

Tanzania kinara EAC

Licha ya mfumuko wa bei kuongezeka kiduchu, Tanzania bado imeendelea kuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Madhariki ambapo Kenya ina asilimia 4.4 na Uganda asilimia 3.5 kwa Mwaka ulioishia Mwezi Agosti.

Enable Notifications OK No thanks