Kasi ya mfumuko wa bei yang’ang’ania kiwango cha Aprili 2024

June 10, 2024 10:56 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasalia asilimia 3.1 kiwango kilichokuwepo mwaka unaishia mwezi Aprili 2024.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia mwezi Mei 2024 imebakia kuwa asilimia 3.1 sawa na kiwango kilichorekodiwa mwaka unaoishia Aprili mwaka huu.

Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Juni 10, 2024 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa hali hiyo imechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei katika baadhi ya bidhaa za chakula na kupungua kwa mfumuko wa bei kwa bidhaa zisizo za chakula.

“Kasi ya Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2024 kuwa sawa na kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi April, 2024 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula,” imesema taarifa ya Nbs.

Kwa mujibu wa NBS  hali hiyo inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2024 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024.

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024 ni pamoja na unga wa ngano kutoka asilimia 1.1 hadi 1.3, samaki pamoja na vyakula vingine vya baharini (kutoka asilimia 5.2 hadi 6.6), dagaa wabichi (kutoka asilimia 1.4 hadi 7.6), mafuta ya kupikia (kutoka asilimia 2.9 hadi 3.7), siagi (kutoka asilimia 1.1 hadi 1.3), mbogamboga (kutoka asilimia 10.1 hadi 12.9) na maghimbi kutoka asilimia 1.8 hadi 2.8.


Soma zaidi:Bei ya petroli, dizeli yashuka kiduchu Tanzania


 “Kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024 ni pamoja na vinywaji vikali na tumbaku kutoka asilimia 4.0 hadi 3.4, nguo za wanaume (kutoka asilimia 2.8 hadi 2.7), nguo za wanawake kutoka asilimia 2.5 hadi 2.2…

…Nguo za watoto kutoka asilimia 2.2 hadi 2.0, viatu vya wanaume (kutoka asilimia 2.2 hadi 1.9),  vifaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa jengo (kutoka asilimia 3.2 hadi 3.0) samani za nyumbani (kutoka asilimia 4.8
hadi 4.6),  petroli (kutoka asilimia 2.1 hadi 2.0) na simu janja kutoka asilimia 3.6 hadi 2.3,” imefafanua taarifa ya Nbs.

Maumivu Kenya, Uganda

Wakati Tanzania kukiwa na ahueni kiasi baada ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Mei 2024, kutobadilika, nchini Uganda mfumuko huo umefikia asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.2  iliyorekodiwa kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024.

Kwa upande wa Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2024 umeongezeka hadi asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2024.

Kiwango hicho kinaifanya nchi ya Kenya kuwa na kurekodi kiwango kikubwa zaidi cha mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Mei, 2024 kulinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki

Enable Notifications OK No thanks