Malima: Ongezeni kasi kilimo cha umwagiliaji kukabiliana mabadiliko tabianchi
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akikata utepe kuzindua maonyesho ya wakulima, wavuvi na wafugaji yanayofanyika katika viwanja vya Nyamgholo jijini Mwanza. Picha | Mariam John.
- Azitaka halmashauri za Mkoa wa Mwanza kuweka msisitizo katika kilimo hicho.
- Asema ni hekta 1,635 kati ya hekta 36,000 ndiyo zinatumika kwa umwagiliaji.
- Kilimo hicho kitasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mwanza. Serikali imezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza kuhakikisha zinaanzisha na kuweka msisitizo katika kilimo cha umwangiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa chakula.
Pia halmashauri hizo zimetakiwa kuwahamasisha wakulima kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo wanapolima mazao ya chakula na biashara ili kuongeza tija ya uzalishaji.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima akizungumza Agosti 4 wakati akifungua Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane, 2022 Kanda ya Ziwa Magharibi, amesema mkoa huo una eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji linalokadiriwa kufikia hekta 36,000.
Kati ya eneo hili hekta 1,635 tu sawa na asilimia 4.5 ndizo zinatumika katika kilimo cha umwagiliaji.
“Fursa hii ikitumika vema inaweza kutoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo katika kuitumia fursa ya uwepo wa Ziwa Victoria katika Kanda ya Ziwa Magharibi na pia kutekeleza uchumi wa bluu,” amesema Malima.
Sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi ndizo zinazoajiri nguvukazi kubwa hapa nchini kuliko sekta zingine ambapo inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 63 hadi 65 ya nguvukazi imeajiriwa na hutegemea kupata riziki katika sekta ya Kilimo.
Malima amesema uwekezaji katika sekta ya kilimo utasaidia sana kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza pato la Taifa na kupunguza umaskini katika Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Amesema kupitia kauli mbiu ya ‘Ajenda 10/30, Kilimo ni biashara, Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipamgo Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ‘ inakumbusha wananchi na wakulima kwamba Serikali inalenga kuona sekta ya kilimo inakuwa kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030.
Mkuu huyo wa Mkoa amezitaja fursa zilizopo Kanda ya Ziwa Magharibi zinaweza kuchangia katika ukuaji wa Sekta ya Kilimo, mathalani Ziwa Victoria linaweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa ukame pamoja na ufugaji wa samaki hasa kwa njia ya vizimba.
Hadi kufikia Agosti 3,2022 idadi ya washiriki wa Maonyesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane, 2022, Kanda ya Ziwa Magharibi walikuwa zaidi ya 228 ikijumuisha Mamlaka za Serikali za Mitaa wenye shughuli kubwa na za kati, taasisi za fedha elimu, afya, kampuni za zana za kilimo, usambazaji pembejeo vinywaji na kampuni za mawasiliano.
Latest
