Mbowe, wenzake waachiwa huru Tanzania

March 4, 2022 9:49 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya DPP kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.
  • Walikuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi.

Dar es Salaam. Baada ya kusota gerezani kwa zaidi ya miezi minane hatimaye Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu wameachiwa huru leo baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo la ugaidi. 

Mbowe na wenzake watatu Khalfani Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya wameachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021.

Wakili kiongozi wa kesi hiyo Peter Kibatala amewaambia wanahabari nje ya mahakama hiyo jijini Dar es Salaam leo Machi 4, 2022 kuwa hati hiyo ijulikanayo kama ‘Nolle prosequi’ inampa mamlaka DPP ya kufuta kesi iliyopo mahakamani katika hatua yoyote ambayo inakuwa imefikia.

Leo Mbowe na wenzie walipaswa kuanza kujitetea mahakamani hapo baada ya mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu Februari 18, 2022.

Washtakiwa katika kesi hiyo, iliyovuta hisia tofauti za watu wengi tangu ianzwe kusikilizwa, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi.

Mashtaka mengine ni kushiriki kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria.

Katika kesi hiyo, Mbowe anadaiwa kula njama ya kutenda kosa la ugaidi kati ya Mei na Agosti mwaka 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro, kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi kati ya tarehe hizo tajwa.

“Kesi hii haikuwa ndogo na madhara yake yangeweza kuwa makubwa kwao (washtakiwa) hasa wale vijana ambao walikuwa na vitu vingi vya kupoteza,” amesema Kibatala. 


Soma zaidi:


Baada ya habari za kuachiwa huru kwa Mbowe wafuasi waliokuwa wamefika mahakamani hapo walikuwa wakishangilia kwa furaha kuachiwa kiongozi wao ambaye hakuwepo eneo hilo. 

Video zaidi kutoka Chadema zinaonyesha mawakili wa kiongozi huyo wa upinzani walivyopongezana kwa kukumbatiana na kushangilia mara baada DPP kuwasilisha hati hiyo ya kufuta mashtaka hayo. 

Mbowe alikamatwa pamoja na wafuasi wengine wa Chadema jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 siku akijiandaa kufanya kongamano la kudai katiba mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na baadaye kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.

James Mbowe, mtoto wa Mbowe amesema wamefurahia kuona  baba yao ameachiwa huru licha ya maumivu waliyonayo ya kutokuwa naye kwa kipindi alichokuwa gerezani.

“Katika yote hayo tunasema wakati wa Mungu ni wakati sahihi, safari hii haikuwa nyepesi maana ni kama wote tulikuwa tumefungwa… sisi upande wa familia lakini  (na) Wanachadema kwa sababu asubuhi mnaamka mnakuja mahakamani,” amesema James. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW