Maumivu, kicheko Ewura ikitangaza bei kikomo za mafuta Novemba 2019
Mbali na mafuta yaliyoingizwa kupitia Dar es Salaam, mafuta yaliyoingiziwa katika Bandari za Mtwara na Tanga yameshuka bei, jambo linalowaokoa pia wakazi wa maeneo hayo kutokutoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hizo muhimu kwa ajili ya usafiri, viwanda na nishati. Picha|Mtandao.
Bei za mafuta mwezi Novemba zimeshuka na kupanda kwa viwango tofauti, jambo litakalowafanya baadhi ya watumiaji kutoboa mifuko yao zaidi na wengine kuneemeka na bidhaa hiyo.
- Bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imepanda kwa Sh98 kwa lita huku ile ya dizeli ikipanda kwa Sh49 kwa lita.
- Mafuta yaliyoingiziwa katika Bandari za Mtwara na Tanga yameshuka bei isipokuwa mafuta ya taa.
Dar es Salaam. Baadhi ya Watumiaji wa vyombo vya moto nchini sasa watakuwa na maumivu baada ya bei za mafuta mwezi Novemba kupanda kwa viwango tofauti ikilinganishwa na mwezi uliopita, zikichagizwa na mabadiliko ya bei ya nishati katika soko la dunia na gharama za usafirishaji wa bidhaa hiyo.
Bei mpya kikomo zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) zinabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imepanda kwa Sh98 kwa lita huku ile ya dizeli ikipanda kwa Sh49 kwa lita.
Maumivu hayo yameenda hadi katika mafuta ya taa ambayo bei yake imepanda kwa Sh62 kwa lita.
“Kwa kiasi kikubwa, mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani kwa mafuta yaliyoingizwa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam yanatokana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta (BPS premiums) na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko dunia,” inaeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa leo (Novemba 5, 2019).
Mbali na mafuta yaliyoingizwa kupitia Dar es Salaam, mafuta yaliyoingiziwa katika Bandari za Mtwara na Tanga yameshuka bei, jambo linalowaokoa pia wakazi wa maeneo hayo kutokutoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hizo muhimu kwa ajili ya usafiri, viwanda na nishati.
Ewura inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga imepungua kwa Sh104 kwa lita, dizeli imeshuka kwa Sh16 kwa lita.
Mafuta hayo hutumiwa na wakazi wa mikoa ya Kaskazini mwa nchi ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro, na Manyara.
Wakazi wa mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wao nao watafaidika na punguzo la bei za rejareja kwa petroli japo ahueni hiyo haitawahusu watumiaji wa dizeli ambayo bei imeongezeka huku mafuta ya taa wakitakiwa kutumia shehena ya mafuta yaliyopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Bei kikomo ya rejareja kwa petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga imeporomoka kwa Sh88 kwa lita huku dizeli ikiongezeka kwa Sh1 kwa lita.
“Kwa kuwa hakuna mafuta ya taa yaliyopokelewa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa (Lindi, Mtwara na Ruvuma) tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Ewura.
Ewura imeeleza kuwa kwa mafuta yaliyoingia nchini kupitia bandari za Tanga na Mtwara, mabadiliko ya bei za mafuta hayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na kushuka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta na punguzo la bei za mafuta hayo katika soko la dunia kwa mwezi Septemba 2019 ikilinganishwa na zile za mwezi Julai 2019, zilizokuwa zikitumika tangu shehena ya mwisho kupokelewa katika bandari hizo.
Taarifa ya Ewura imeeleza kuwa bei hizo mpya zinaanza kutumika kuanzia kesho (Novemba 6, 2019) nchini kote.
Hata hivyo, kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na kanuni (formula) iliyopitishwa na EWURA.
Latest
