Maumivu, kicheko: Bei za vyakula zikipanda Mwanza

October 14, 2022 7:40 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wafanyabiashara, watumiaji wasema bei siyo himilivu.
  • Wakulima waendelea kuneemeka.
  • Serikali yasema inachukua hatua kudhibiti mfumuko wa bei.

Mwanza. Bei za vyakula na bidhaa mbalimbali mkoani Mwanza zimeendelea kupanda huku wafanyabiashara na watumiaji wakiiomba Serikali kuangalia namna ya kudhibiti mfumuko wa bei.

Tofauti na miaka ya nyuma, bei za mbogamboga zimeonekana kupanda katika kipindi hiki huku sababu ikitajwa kuwa ukame unasababishwa na kuchelewa kuanza kwa mvua. 

Baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Buhongwa jijini hapa wamesema iwapo hali ikiendelea kuwa hivi bei za vyakula na mbogamboga itaendelea kupanda zaidi.

“Changamoto kubwa ni ukosefu wa mvua, wanaolima bustani wanategemea mvua zinyeshe malambo na visima vijae ili waweze kumwagilia lakini hivi sasa mvua imechelewa kuanza.

Malambo na visima vimekauka hali inayosababisha wakulima kushindwa kupata maji ya kumwagilia,” amesema Hellen Masanja, mfanyabiashara wa mbogamboga katika soko la Buhongwa.

Kabla ya bei hizo kupanda walikuwa wanauza fungu moja la mboga kwa Sh200 na zilizokatwakatwa wanapima kuanzia sh300, anasema Masanja “lakini sasa hali ni tofauti, zilizokatwa tunapima kuanzia Sh500 na ambazo hazikukatwa tunauza Sh300.”

Pia mfumuko huo wa bei unaonekana kwa vyakula kama mahindi na maharage huku wafanyabiashara wakieleza huenda bei zikapanda zaidi ya hapo.

Elias Makoye ni mfanyabiashara wa duka la nafaka katika soko la Buhongwa amesema kwa sasa kilo moja ya mchele supa wanauza Sh2,800 kutoka Sh2,200 miezi mitatu iliyopita huku mchele wa kawaida wakiuza Sh2,200 hadi sh 2,500 na inategemea na aina ya mchele.

Bei za maharage pia zimepanda kutoka Sh2,000 miezi mitatu iliyopita na kufikia Sh3,000 kwa kilo moja huku ndegu na choroko pia zimepanda kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000.

“Sababu kubwa ninayoiona ni kwa kuwa hivi sasa mipaka iko wazi hivyo vyakula vingi vinauzwa nje ya nchi, lakini kukosekana kwa mvua kunachangia bei hizi kupanda,” amesema Makoye.

Wafanyabiashara wa mahindi wakiendelea na biashara zao eneo la Buhongwa jijini Mwanza. Picha | Mariam John. 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wiki hii ilisema kuwa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma muhimu umepanda hadi asilimia 4.8 mwaka unaoishia Septemba 2022 kutoka asilimia 4.6 ya mwaka unaoishia Agosti 2022.

Thobietha Emmanuel yeye ni mfanyabiashara wa mahindi anasema kwa sasa hali ni ngumu, bei za mahindi zimepanda na huenda zikaendelea kupanda zaidi ya hapo.

Anasema pamoja na kwamba mahindi yanauzika ni kwa kuwa ni chakula na watu hawawezi kuka na njaa inawalazimu kununua hata kama bei iko juu.

“Kiuhalisia bei iko juu, biashara ni ngumu ingawa watu wanalazimika kununua, sado moja ya mahindi inauzwa Sh4,800 kutoka Sh2,500 miezi mitatu iliyopita, na hali ikiendelea hivi ya mvua kutonyesha huenda bei zikapanda zaidi ya hapa na kufikia Sh7,000 kwa sado bei ambayo haijawahi kufikiwa toka miaka na miaka,” amesema Emmanuel.

Anasema debe moja la mahindi linauzwa Sh25,000 kutoka Sh12,500 miezi mitatu iliyopita huku gunia likiuzwa kati ya Sh148,000 hadi Sh150,000 na inategemea na aina ya aeneo husika.

‘Ni maumivu tu’

Baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa zisizo za vyakula ikiwemo nguo wanalalamika kukosa wateja kwa sababu wateja wamepungua na pesa zao zinatumika kununua vyakula.

“Tunasubiria siku za sikuu huenda mambo yakabadilika kidogo lakini kiuhalisia kwa sasa hali ni ngumu kuna siku tunafunga biashara hata kuuza nguo moja hamna,” amesema Meshack Philipo, mfanyabiashara jijini hapa.

Amependekeza kuwa Serikali iangalie namna ya kushusha bidhaa za vyakula ili unafuu uwepo kwa watumiaji na wauzaji.


Soma zaidi:


Vipi kwa watumiaji hali ipoje?

“Hali ni mbaya kila kukicha afadhali ya jana, hela imekuwa ngumu tunashindwa tushike nini tuache nini kwa kweli maisha yamepanda sana, ule msemo wa laki si pesa unajidhihirisha wazi,” amesema Iman Abel, mkazi wa Mkolani jijini Mwanza

“Mfano kilo moja ya mchele Sh2,800, mboga labda tuseme nyama nusu kilo Sh4,000, bado mafuta na viungo vingine na kiuhalisia watu sita hawawezi kula kilo moja ya mchele wakashiba,” amesema Abel.

Amesema bei hizo zinawaumiza watu hasa wale wenye kipato cha chini ambapo mtu anashindwa namna ya kuigawa pesa ili iweze kutosheleza mahitaji ya kila siku.

Aman ameishauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza bidhaa za vyakula ili kuleta unafuu kwa wananchi na ikiwezekana mipaka ifungwe ili kulinda vyakula vilivyopo.


Tangazo


Kauli ya viongozi 

Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mwanza, Ahmed Nchora amekiri bei za bidhaa kupanda huku sababu akitaja kuwa ni kupungua kwa vyakula kwenye maghala ya wakulima.

Nchora amesema sababu kubwa ya bidhaa kupanda ni msimu wa kilimo ulioisha kutokuwa mzuri kutokana na mvua kuwa chache hivyo uzalishaji kuwa mdogo.

Amesema wakulima wengi hutegemea mvua na hawalimi kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika, hivyo uzalishaji kuwa hafifu.

Hivi karibuni Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dk Ashatu Kijaji alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua kuwapunguzia wananchi athari zinazotokana na kupanda kwa bidhaa muhimu.

Alizitaja hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa mbalimbali, ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mahitaji muhimu kama chakula kutoka nje ya nchi.

Hatua nyingine ni kuthibiti upandaji holela wa bei na hivyo bei ya bidhaa kwenye soko la ndani zimeendelea kuwa na utulivu, kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ya kupikia yaliyosafishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW