Kuelekea msimu wa sikukuu, bei za vyakula zapaa sokoni

December 2, 2021 1:46 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni katika soko kuu la Mwanza.
  • Ukame, maandalizi ya sikukuu vyachangia.
  • Wafanyabiashara watumia fursa hiyo kujinufaisha.

Mwanza. Wakati wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ukikaribia, bei za vyakula katika baadhi ya masoko likiwemo soko kuu la jijini Mwanza zimeanza kupanda, jambo linaloweza kuwaumiza walaji.

Bei za vyakula ambazo zimepanda katika soko hilo linalotegemewa na wakazi wengi wa Mwanza ni pamoja na mboga mboga, mchele, maharage na kuku.

Hali hiyo imechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa vyakula vilivyokuwa vimehifadhiwa na wakulima ghalani.

Mwenyekiti wa soko kuu jijini Mwanza, Ahmed Nchora akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ametaja sababu nyingine ni kutokana na msimu wa kilimo kugubikwa na ukame kwa kipindi kirefu hali inayosababisha wakulima kutolima na kuvuna mazao yao kwa wakati.

Nchora amesema wakulima wengi huanza kulima kati ya mwezi Oktoba na kufikia Februari wanaanza kuvuna na kuwa mwaka huu hali ni tofauti ambapo wakulima wengi hawajaanza kuvuna.

Sababu nyingine ni  kuanza kwa maandalizi ya msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwemo Krismas ambapo mara nyingi bei ya baadhi ya  vitu huwa vinapanda.

Mwenyekiti huyo ametaja bei ya mchele kupanda kwa zaidi ya Sh200 kwa kilo moja kwa mchele supa huku bei ya mchele wa kawaida ukipanda kwa zaidi ya Sh300 kwa kilo moja.

“Awali bei ya mchele wa kawaida ulikuwa unauzwa Sh1,200 kwa kilo moja na sasa unauzwa kati ya  Sh1,500 hadi 1,650 huku bei ya mchele supa ukiuzwa kati ya Sh1,800 kutoka Sh1,600 ya awali,” amesema Nchora.

Akizungumzia kupanda kwa bei ya bidhaa nyingine ikiwemo maharage na kuku, Nchora amesema kwa sasa bei ya kuku wa kawaida anauzwa Sh15,000 hadi Sh20,000  kutoka Sh10, 000 kwa bei ya zamani.

Bei za maharage pia zimepanda kutoka Sh1,600 kwa kilo hadi Sh1,800 hadi Sh2,000 kwa kilo huku bei ya viazi mviringo nayo ikipanda kutoka Sh650 kwa kilo na kufikia Sh800.

“Tunaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara wasipandishe sana bei hususani kuku ili wasifukuze wateja kwa kuwa hivi sasa wateja wengi wanakuja masokoni tofauti na kipindi kilichopita ambapo wafanyabiashara wengi walikuwa barabarani,” amesema Nchora.

Ikiwa bei ya bidhaa za vyakula ikipanda inawafaidisha zaidi wakulima na wafanyabiashara na kuwafanya walaji kutoa mifuko yao zaidi kupata bidhaa hizo.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara hutumia fursa ya sikukuu za mwisho wa mwaka kupandisha bei ili kujinufaisha na kupata faida maradufu huku wakiacha maumivu kwa walaji.

Mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, Said Amir amesema kupanda kwa bei kumetokana na kuongezeka kwa wateja wanaokwenda sokoni baada ya Serikali kuwaondoa wamachinga barabarani.

Amiri anasema hali hiyo imechangia mahitaji ya bidhaa kuongezeka na hivyo kusababisha bei kupanda.

“Na hii ni kwasababu watu waliogopa kuingia sokoni kununua vitu wakiogopa msongamano na kuambukizwa ugonjwa wa corona ambapo watu walikuwa wanakuja kuhemea vyakula vya muda mrefu,” amesema Amir.

Mfanyabiashara mwingine, Kurijila Athuman amesema kwa sasa  biashara imechangamka hivyo ni wakati wao kujipatia bidhaa kwa sababu janga la Corona limepungua.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV