Ahueni, maumivu: Bei za vyakula zikianza kushuka Mwanza

April 18, 2023 5:42 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Wafanyabiashara wa soko la Mbugani wakiendelea kuhudumia wateja, licha ya kasi ya uuzaji kupungua. Picha | Mariam John. 


  • Wafanyabiashara walalamika kasi ya kuuza vyakula yapungua
  • Wananchi wadai ugumu wa maisha wachangia licha ya bei kuanza kushuka.

Mwanza. Baadhi ya wafanyabiashara mkoani Mwanza wamesema kasi ya wateja kununua bidhaa zao imepungua hasa Aprili mwaka huu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, jambo linalochangia bidhaa kuharibika na kukosa faida inayokusudiwa. 

Sababu zinazotajwa kupunguza kasi ya ununuzi ya vyakula ni kutokana na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwarezima ambazo ni nguzo muhimu za waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo.

Katika kipindi hicho, watu wengi hupunguza kula vyakula wakitekeleza masharti ya imani zao. 

Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imezungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa masoko ya Mbugani na Mirongo jijini hapa ambapo wamesema kwa sasa bidhaa zinakosa wateja na wakati mwingine kuharibika na kuwasababishia hasara.

“Kiujumla hali ya biashara ni mbaya, hatuwezi kujua kwenye siku kuu hii ya Eid El Fitri lakini ile ya pasaka ilikuwa mbaya hali iliyosababisha kuku kutouzika,” amesema Mwita Chacha, mfanyabiashara wa kuku katika soko la Mbugani.

Chacha ametaja bei za kuku kwenye soko hilo kuwa ni kati ya Sh10,000 hadi 25, 000 kwa jogoo mkubwa.

Mfanyabiashara mwingine Yunis Aman amesema sababu kubwa inayochangia kuku kupanda ni kutokana na wanakowachukulia kuwanunua  kwa bei ya juu huku sababu ikitajwa ni  kupanda kwa bei ya chakula cha kuku.

Anita Mdogo yeye anajishughulisha na uuzaji wa mihogo na viazi katika soko la Mirongo amesema fungu moja la viazi wanafunga kuanzia Sh1,000 hadi Sh2,000  kwa viazi vikubwa huku fungu la mihogo likiuzwa kwa Sh2,000 hadi Sh3,000.

Amesema viazi vimepanda  kutokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua hali inayosababisha wakulima kutolima zao hilo kwa wingi.

“Mwaka huu hakuna viazi vya kutosha ndiyo maana tunauza kwa bei hiyo,” amesema Mdogo. 


Zinazohusiana:


Mfabiashara wa soko wa Mirongo, Tatu Julius amesema ugumu wa biashara umesababisha pia kushusha kwa kipato chao ambapo zamani walikuwa wakiuza kuanzia Sh300,000 kwa siku lakini kwa sasa wanauza chini ya Sh100,000.

Amesema pia wateja kwa sasa wamepunguza kunua vitu. Mfano, mteja aliyekuwa ananunua kilo tatu hadi nne kwa sasa ananunua chini ya hapo.

“Ni kwa sababu uchumi umeshuka watu hawana hela hali inayosababisha wateja kutomudu kununua mahitaji mengi kwa wakati mmoja,” amesema Julius. 

Akizungumzia changamoto hiyo mwenyekiti wa soko kuu mkoani Mwanza, Ahmed Nchora amesema tofauti na miezi mitatu iliyopita hali ya bidhaa za vyakula kwa sasa imeshuka.

Mwita Chacha, mfanyabiashara wa kuku katika soko la Mbugani. Picha | Mariam John. 

Kwa mujibu wa Nchora, hali hiyo imechangiwa na kuanza kuingizwa kwa chakula kutoka nje ya nchi na baadhi ya wakulima kuanza kuivisha mazao yao.

Amesema awali kilo moja ya mchele iliuzwa Sh3,800 lakini kwa sasa imeshuka na kufikia Sh3,200 kwa kilo moja, huku bei ya nyama ikishuka kutoka Sh8,000 na kufikia Sh6,500 kwa kilo moja.

Bei ya maharagwe pia imeshuka kutoka Sh3,000 na kufikia Sh2,600 kwa kilo wakati kilo ya viazi mviringo ikiuzwa Sh1,000 kutoka Sh1,500.

Nchora amesema hawajapata malalamiko mengi ya vyakula kupanda sana wakati mfungo wa Ramadhan na Kwarezima, licha ya hali ngumu ya maisha inayopunguza kasi ya ununuzi wa vyakula.

“Ni kweli bidhaa zimeshuka lakini wateja hamna hii ni kutokana na hali ngumu ya maisha na ndio maana hata bei za nyama zimeshuka hivyo watu kwa sasa hawatakiwi kula sana ni kidogo tu,” amesema Nchora.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW