Marekani yajibu maswali chanjo ya Johnson and Johnson Tanzania

August 5, 2021 2:09 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wa afya kutoka timu ya Ubalozi wa Marekani wasema chanjo ya Johnson & Johnson ni salama tofauti na inavyoelezwa
  • Waeleza kuwa uzushi unaosambazwa ukiwemo kuwa chanjo hiyo inapunguza nguvu za kiume si wa kweli.

Dar es Salaam. Hatimaye Serikali ya Marekani imetoa ufafanuzi wa mashaka yanayowakabili baadhi ya watu juu ya usalama wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona (Uviko-19) iitwayo Johnson & Johnson ikisema ni salama.  

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa wanafahamu kuwa Watanzania wengi wana wasiwasi juu ya chanjo ya Corona na hawana taarifa za kutosha zitakazo wasaidia kufanya uamuzi sahihi.

“Chanjo ni sehemu muhimu ya nyenzo za afya ya jamii kwa sababu ni salama na zinafanya kazi. Jambo hili ni kweli kwa chanjo za zamani na hata kwa chanjo mpya dhidi ya virusi vya Korona. Sayansi haina hofu kuhusu suala hili,” amesema Wright. 

Wright amesema kwa sasa nchini Marekani, zaidi ya asilimia 99 na vifo vipya vinavyotokana na Uviko-19 ni vya watu ambao hawajachanja. 

“Ukweli mwepesi ni kuwa chanjo hizi zinaweza kuokoa maisha yako au maisha ya mpendwa wako,” amesema Wright.

Chanjo ya Johnson & Johnson ilipokelewa Julai 24, 2021 katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ikiwa msaada kutoka Marekani kupitia mpango wa usambazaji chanjo wa Covax ulioratibiwa na Umoja wa Afrika. 

Mapema Julai 28 Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mpango rasmi wa kuchanja nchini kwa kuchanjwa akieleza kuwa ni salama.   

Katika mkutano huo na wanahabari, wataalamu wa afya kutoka ubalozi huo wameeleza kuwa madai mengi yanayosemwa mitaani juu ya chanjo ya Corona sio ya kweli na hayajathibitishwa kitaalamu.

Hata hivyo, bado kumekuwa na baadhi ya watu wanaoendelea kupotosha ama kutoa nadharia hasi kuhusu chanjo ya Uviko-19 ikiwemo ya Johnson & Johnson ambayo pia hujulikana kama Janssen. 

“Madai mengi yakiwemo chanjo kusababisha ukosefu wa nguvu za kiume kwa wanaume au kusababisha ugumba na utasa sio ya kweli ni madai yanayovuma ila hayana ukweli wowote ndani yake,” amesema Dk Emmanuel Tluway wa Shirika la Misaada kutoka kwa Watu wa Marekani (USAID).

 Wataalam wa afya kutoka timu ya Ubalozi wa Marekani wakizungumza na wanahabari Agosti 5, 2021. Picha | Tulinagwe Malopa.

Amesema kila chanjo ina madhara madogomadogo yasiyokwepeka na kwamba kuna umuhimu mkubwa wa watu kupata chanjo kwa kuwa ni kinga muhimu inayoweza kumsaidia mtu kutokupata maambukizi kwa haraka.

“Chanjo hizi hasa ya Johnson & Johnson ni tiba inayosisimua kinga ya mwili na inamwezesha mtu kujikinga na maambukizi hata kama ina maudhi madogomadogo yasiyokwepeka hata kwenye chanjo za aina nyingine,” amesema Dk Tluway. 

Kwa nini aliyechanjwa anatakiwa kuchukua tahadhari za Uviko-19?

Alipoulizwa iwapo aliyechanjwa hatakiwi kuchukua tahadhari kwa kuwa ana kinga, Dk Arkan Ibwe kutoka U.S Peace Corps amesema chanjo ni kinga inayomsaidia mtu kutokupata maambukizi ya Corona hovyo ila haimaanishi atakaepata chanjo hatatakiwa kuchukua tahadhari zote zilizowekwa za kujikinga na maambukizi mapya ya ugonjwa huo. 

“Chanjo ni kama ulinzi kwenye mwili wa binadamu. Inashauriwa mtu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 hata kama amepata chanjo,” amesema Dk Arkan.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV