Miaka 11 ya vita ya Syria: “Tuchague amani”

March 12, 2022 8:17 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • UN yasema makundi yanayohasimiana yazungumze kuepuka vita zaidi.
  • Ukraine hali bado tete, raia wazidi kuyakimbia makazi yao.

Dar es Salaam. “Mwaka mwingine umepita! Kumbukizi ya kutisha ya vita iliyosambaratisha Syria na watu wake.” Ndivyo anavyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres katika ujumbe wake wa miaka 11 tangu kuanza kwa vita nchini Syria.

Guaterres katika ujumbe wake ulioutoa Machi 11, 2022 amesema kipindi hicho kimekuwa cha mapigano ya kikatili ambayo yamekuwa na gharama isiyopimika kwa binadamu kwa kuwa Wasyria wamegubikwa na ukiukwaji wa kiwango cha juu kabisa wa haki za binadamu.

“Uharibifu ambao Wasyria wamepitia ni wa kiwango kikubwa na mbaya zaidi unaoweza kulinganishwa na matukio katika historia ya zama za dunia ya sasa,” amesema na kubainisha kuwa,

“Uharibifu ambao vita hiyo imesababisha kwenye miundombinu umeongeza janga la kiuchumi na kufanya mahitaji ya kibinadamu kufikia kiwango cha juu zaidi tangu kuanza kwa mzozo huo wa kivita.”

Mamilioni ya wakimbizi wa ndani na wakimbizi wanahaha kuishi katika mazingira magumu, amesema Guterres.

Vita nchini Syria ilianza Machi mwaka 2011 ambapo vimewalazimisha zaidi ya nusu ya raia wa nchi hiyo kuyakimbia makaazi yao na kusaka hifadhi kwengineko duniani, wengi wao kwenye mataifa jirani, hasa Uturuki.

Majengo yaliyoharibiwa kwa makombora kwenye mji wa mashariki wa Aleppo nchini Syria. Yadaiwa silaha za kemikali zilitumika kwenye mashambulizi. Picha| OCHA/Halldorsson.

Suluhu hii hapa

“Katu hatupaswi kukata tamaa. Tunapaswa kuchukua  hatua sasa. Lazima tuoneshe ujasiri na azma ya kuchukua hatua zaidi ya kauli za hovyo ili kuleta amani na kuchukua hatua zote ili kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2254 la mwaka 2015 kuhusu suluhu ya kisiasa Syria inayoongozwa na Wasyria wenyewe,” amesema.

Katibu Mkuu huyo amesema njia hiyo ndio suluhu inayoweza kukidhi matamanio na kuweka mazingira chanya kwa raia wa Syria walio ukimbizi kurejea nyumbani kwa hiari, katika mazingira ya utu na kwa usalama.

Guterres amehitimisha ujumbe wake akisema, “ujumbe wangu ni dhahiri: Hatuwezi kuwaangusha wananchi wa Syria. Mapigano lazima yakome. Natoa wito kwa pande zote zishiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa na natoa wito tufanikishe upelekaji wa misaada ya kibinadamu. Lazima tuchague amani.”


Soma zaidi:


Ukraine hali bado tete

Katika muda wa wiki mbili, zaidi ya watu milioni 4.4 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano ya Ukraine baada ya nchi hiyo kuvamiwa na Urusi.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), watu milioni 1.85 wamekimbia makazi yao ndani ya Ukraine na wengine zaidi ya milioni 2.5 wamevuka mipaka ya kimataifa ya Ukraine. 

Jumla ya watu wote walioathirika na mzozo huo wa Ukraine hadi sasa ni milioni 12.65 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu masuala ya Kibinadamu (OCHA) pia imeripoti kuwa maeneo makubwa ya ya wakimbizi wa ndani yapo magharibi na kaskazini magharibi mwa Ukraine.  

Maeneo hayo ni pamoja na Zakarpatska, yenye wakimbizi wa ndani zaidi ya 500,000, Lvivska  wakimbizi 387,000 na Volynska wakimbizi 170,000. 

Machi 5, 2022 mashariki mwa Ukraine, watoto na familia wakielekea katika mpaka kuvuka kuingia Poland. Picha| UNICEF/Viktor Moskaliuk.

“Watu waliotawanywa ambao wengi ni wanawake, watoto na wazee  wanakabiliwa na hatari kubwa za ulinzi na wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu wa aina mbalimbali kulingana na mahitaji yao maalum,” OCHA imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni ya hali ya kibinadamu nchini Ukraine iliyotolewa  Machi 10, 2022. 

Hadi sasa, Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wake wametoa msaada wa kibinadamu kwa zaidi ya watu 500,000 nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na chakula cha kuokoa maisha, malazi, blanketi na vifaa vya matibabu. 

Kwa upande wake, shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) linapanga kusaidia hadi watu milioni 3.1.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW