Mambo yatakayosaidia kuendeleza wanawake katika sayansi

February 11, 2022 8:31 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja kuzingatia matamko ya kimataifa kuhusu sayansi.
  • Kuhimiza usawa wa kijinsia.
  • Wanawake wapewe fursa zaidi katika sayansi.

Dar es Salaam. Wakati leo dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, wadau wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) wametakiwa kuzingatia matamko mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kuhakikisha elimu inachangia katika maendeleo endelevu.

Tume ya Taifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania imesema matamko hayo yaatoa dira ya kufikia malengo ya kuwasaidia wasichana kutimiza malengo yao katika sayansi.

Kaimu Naibu Mtendaji upande wa Programu wa Tume hiyo, Fatma Mrope ametoa kauli hiyo alipozungumza kwa njia ya mtandao na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania.

“Kupitia hayo matamko ya kimataifa ndiko ambako unakuta ripoti mbalimbali. Kwa mfano sasa hivi kuna ripoti ya mstakabali wa elimu. Kwa hivyo vitu kama hivyo ndivyo vitatufanya na sisi tusibakie nyuma. 

Amesema sasa hivi dunia imefikia hatua ambayo kipaumbele ni kujadili inayoleta maana kwa maisha ya wasichana na wanawake.

“Kwa hivyo sasa hivi tunazungumzia elimu ya maendeleo endelevu. Hata tunapoadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi ni wajibu wetu pia kutafakari hayo mengine yanayohusiana na muktadha mzima wa sayansi na elimu,” amesema Mrope.

Mrope amesema kwa upande wake tume hiyo hata kabla ya kuanza kwa maadhimisho haya miaka sba iliyopita imekuwa ikichukua kuhamasisha wanawake na wasichana kwa kuwa na dawati la wanasayansi wanawake.  

“Ukiacha dawati la wanasayansi wanawake, lakini pia tumekuwa na utaratibu wa kuhamasisha kupitia taarifa za jamii ya kimataifa. Kuna programu ambayo imeanzishwa katika muktadha wa kijinsia zaidi. Katika kuitekeleza kwetu tulienda Karatu (mkoani Arusha),” amesema Mrope. 

Aidha, ameitaka jamii kuhimiza zaidi usawa wa kjinsia kwa wasichana na wavulana ili kuwawezesha utimiza ndoto za elimu. 

“Watoto wenyewe wanasoma bailojia, wanasoma kwa hiyo wanasoma katika lile somo la jenetiki. Vinasaba vile vinavyotoka kwa wazazi, ukiacha vile vinavyotuletea utofauti basi vingine mgawanyo wake huwa hamna kusema huyu atakuwa hivi huyu atakuwa hivi.

“Katika hali kama hiyo, tunakuwa na uwezo sawa wa kuweza kufafanua mambo mbalimbali katika mchakato wa elimu.  Kwa hiyo niwape moyo watoto wa kike kwamba wanaweza na wanaweza kufika sehemu mbalimbali katika ngazi mbalimbali kupitia sayansi,” amesema Mrope.


Zinazohusiana:


Mambo mtambuka

Wakati ulimwengu unaendelea kukabiliana na Uviko-19 na mabadiliko ya hali ya hewa, ushiriki kamili na sawa na uongozi wa wanawake na wasichana katika jamii za sayansi na teknolojia ni muhimu zaidi kwa wakati huu.

Ni wakati wa kutambua michango ya wanawake katika utafiti na uvumbuzi, kuvunja dhana potofu na kushinda ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana katika sayansi.

Taasisi ya Takwimu ya Unesco (UIS) inaeleza kuwa asilimia 30 tu ya watafiti ni wanawake, na wanatunukiwa ufadhili mdogo wa utafiti kuliko wanaume, na wana uwezekano mdogo wa kupandishwa cheo. 

Pia UIS inaeleza kuwa wanawake wanachangia asilimia 22 tu ya wataalamu wanaofanya kazi katika akili bandia na asilimia 28 ya wahitimu wa uhandisi. 

Uwakilishi huu mdogo huzuia uwezo wa dunia kupata masuluhisho jumuishi, endelevu kwa matatizo ya kisasa na kujenga jamii bora kwa wote.

Mwaka jana, katika Kongamano la Usawa wa Kizazi lililofanyika Ufaransa, Muungano wa Utekelezaji wa Teknolojia na Ubunifu ulizinduliwa, ukizileta pamoja serikali, makampuni ya sekta binafsi, mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia ili kutoa ahadi thabiti kwa wanawake na wasichana katika STEM. 

Wadau wa muungano huo wanalenga kuongeza maradufu uwiano wa wanawake wanaofanya kazi katika teknolojia na uvumbuzi ifikapo 2026, na kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu kwa matatizo makubwa na magumu zaidi ya maisha duniani. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW