TCRA yawanoa wasichana kujiingiza katika masomo ya sayansi
- Yatoa mafunzo ya Tehama kwa siku tano kwa wasichana waliopo mashuleni, vyuoni.
Arusha. Kuelekea siku ya wasichana katika Tehama, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mafunzo kwa wasichana 25 nchini ikiwa ni jitihada za kuongeza ujumuishi wa kijinsia katika tasnia hiyo.
Wasichana hao kutoka ngazi ya shule za awali msingi, sekondari na vyuo watapata mafunzo hayo kwa siku tano kuanzia Machi 24 hadi 28, 2025 na baadae kushindanishwa kubuni mifumo ya Tehama itakayotatua changamoto za kijamii.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari, aliyekuwa akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo yanayoratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na wakufunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) amewahimiza washiriki waliochaguliwa kutoka taasisi za elimu ya juu kuweka juhudi katika mafunzo ya uchakataji wa taarifa (Data Science) ili kuweza kushiriki kikamilifu katika Uchumi wa Kidijiti.
Miaka ya hivi karibuni Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya jitihada za kuongeza idadi ya wasichana wanaosoma masomo ya sayansi ili kuongeza usawa wa kijinsia katika tasnia hiyo.
Miongoni mwa jitihada hizo ni ujenzi wa shule za michepuo ya sayansi kwa ajili ya wasichana ikiwemo Shule Maalum ya Wasichana Kilindi jijini Tanga iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Wasichana wakipata mafunzo ya Tehama katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Picha| TCRA/Instagram.
Akizungumza baada ya kuzundua shule hiyo Rais Samia alisema Serikali imefanikiwa kujenga shule za sayansi za wasichana katika mikoa yote 26 na sasa inajielekeza kujenga shule za mchepuo huo kwa wavulana.
Pamoja na jitihada hizo za kitaifa, TCRA imekuwa ikiendesha mafunzo hayo ya sayansi kwa miaka saba mfululizo tangu maadhimisho hayo yaanzishwe rasmi na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU).
Mafunzio hayo ni miongoni mwa shamra shamra za kuadhimisha siku ya wasichana katika Tehama ambayo huadhimishwa Aprili 25 kila mwaka lengo likiwa ni kuwahamasisha na wasichana na wanawake kupenda masomo Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM) ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hasa lengo namba 5.
Latest



