Esther Mndeme: Muongozaji aliyewashangaza wengi tuzo za filamu 2019

Zahara Tunda 0633Hrs   Machi 06, 2019 Ripoti Maalum
  • Mndeme amepata tuzo tatu za filamu kwa tamthilia ambayo bado haijapata mnunuzi wa kuionyesha kwenye televisheni.
  • Anaingia kwenye rekodi za waongozaji wachache wa filamu wanawake nchini waliopata heshima katika tasnia hiyo.
  • Pamoja na uwezo wake kikazi bado anakabiriwa na changamoto za kuweza kuchomoza katika biashara ya filamu iliyotawaliwa na wanaume. 

Kwa wapenzi wa filamu na tamthilia, usiku wa tuzo za Sinema Zetu International Film Festival 2019 (SZIFF) zilizofanyika hivi karibu huenda uliwashangaza wengi. 

Ukiachana na watoto Rashid Msigala (10) na Flora Kihombo (11) kutoka Iringa walioshinda tuzo za mwigizaji bora wa kiume na wa kike maarufu “Kina kamwene” kuna mtu mwingine ambaye huenda pia aliwashangaza wengi.

Huyu si mwingine bali ni muongozaji filamu Esther Mndeme  ambaye amekuwa akitumia tasnia hiyo kuleta mabadiliko katika jamii na kumweka katika hatua nzuri za kukua katika biashara ya tasnia hiyo. 

Esther anawakilisha wanawake wachache katika uongozaji wa tamthilia na filamu na unaweza kumfananisha kama Angelina Jolie muigizaji maarufu wa filamu ambaye kabla ya uigizaji alikuwa mwongozaji wa filamu. Kwa sasa Jolie ni moja ya waigizaji na waongozaji waliojiwekea heshima kubwa katika soko la filamu duniani. 

Lakini kabla ya usiku wa Februari 23, 2019 wengi hawakuwa wanamfahamu Esther Mndeme (30) mpaka alipoibuka kuwa mwongozaji bora wa tamthilia ya Safari Yangu katika tuzo hizo za SZIFF ambayo mpaka sasa bado haijaanza kurushwa katika stesheni yoyote.

Ushindi huu wa Esther sio kitu pekee kilichofanya Nukta kumtafuta bali ni uwezo wake wa kufanya makubwa katika filamu ikilinganishwa na umri wake katika tasnia iliyotawaliwa na wakongwe wengi wakiwa ni wanaume. 

Tangu aanze kutayarisha filamu na tamthilia, Esther aliyesomea utayarishaji filamu na uigizaji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amefanikiwa kuongoza filamu fupi mbili na tamthilia moja ambazo zote zimejikita kuonyesha mateso anayoyapata mtoto wa kike na jitihada zinazohitajika kumkomboa katika ukatili wa kijinsia. 

Esther Mndeme wakati wa tuzo za SZIFF 2019 mwishoni mwa Februari mwaka huu. Picha|Hisani ya Esther Mndeme.

Kutokana na umahiri wake wa kugusa jamii kwa filamu fupi, amefanikiwa kupata tuzo mbalimbali za kimataifa zinazotambua watayarishaji na waigizaji filamu wanaofanya vizuri katika shughuli zao. 

Mafanikio yake yalianza kuchomoza mwaka 2018 pale filamu yake ya Leah ilipotambuliwa kama filamu fupi bora.  

“Mwaka 2018 filamu fupi yangu inayoitwa Leah ambayo imejikita kuzungumzia athari za ukeketaji kwa watoto wa kike ilishinda tuzo za Zanzibar International Film Festival (ZIFF) kama Filamu fupi Bora (Best Short Film 2018),” amesema Mndeme.


Zinazohusiana: 


Mwaka huu tena, Mndeme hakufanya makosa, amewatoa kimaso maso wanawake wakati wakijiandaa kusherehekea siku yao Machi 8 ambapo amepata tuzo tatu kutokana na tamthilia yake ya ‘Safari Yangu’ katika SZIFF zilizotolewa Februari 23, 2019.

Tuzo hizo ni ile muongozaji bora wa filamu, filamu iliyohaririwa vizuri (Best editing) na filamu bora (Best Series), ambapo ameiambia Nukta kuwa amepata tuzo hizo kwa sababu anaamini kuwa Majaji waliona kazi zake ni nzuri katika nyanja zote.

Licha ya kuwa na uthubutu wa kupeleka tamthilia  ya Safari Yangu  katika kinyang’anyiro cha tuzo za SZIFF, bado haijaingia sokoni rasmi kutokana na kutopata mteja ambaye  ataweza kuinunua na kuirusha kwenye stesheni yake.

Akielezea kuhusu tamthilia yake ya Safari Yangu  iliyompatia tuzo, anasema imejikita kuzungumzia rushwa, mimba za utotoni, madawa ya kulevya, na unyanyasaji wa kijinsia.

Ili Mndeme aendelee kusonga mbele, anatakiwa kukabiliana na changamoto za soko hasa kutokukubalika kwa waandaaji wa changa wa filamu ambao hawana majina makubwa ikizingatiwa kuwa televisheni nyingi huangalia watu wenye majina makubwa wa kufanya nao kazi.

Ugumu wa soko kupokea kazi za waandaji wadogo kama Esther, kunawafanya washindwe kukua kibiashara licha ya ubora wa kazi wanazofanya.

“Hali hiyo inatunyima sisi ambao hatuna majina tunapitia wakati mgumu sana kufikisha kazi zetu za sanaa kwa jamii,” amesema Mndeme.

Pia, ana kibarua kigumu cha kutengeneza hadhira ya mtandaoni ili kuwafikia watu wengi wanaotumia mitandao ya kijamii, ikizingatiwa kuwa bado hajaanza kuwafikia watumiaji hao.

“Mimi nachoweza kuwaambia ni kwamba, tunaweza muhimu ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kujiamini,” anasema Mndeme ikiwa ni salamu yake kwa wanawake wenye uthubutu katika jamii. 

Related Post