Kutana na wanasayansi wa kike wanaotikisa mashindano ya ulimbwende Tanzania

October 29, 2019 8:35 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kusoma masomo ya sayansi hakukunyimi fursa ya kushiriki shughuli nyingine za kijamii kama mitindo na ulimbwende.
  • Sarafina Wasley na Elverenta Reuben, ni mabinti walijikita katika masomo ya udaktari na uhandisi lakini bado wanafanya vizuri kwenye mashindano ya ulimbwende.
  • Ujasiri wa kufanya kile wanachokipenda umewafanya kuzishinda changamoto na kutengeneza kipato na mtandao wa ndoto zao.  

Dar es Salaam. Jukwaani, warembo wa Tanzania walianza kuikanyaga barabara ya wanamitindo wakivalia michuchumio iliyowaongezea urefu kama wa Twiga, mavazi yaliyowafananisha na malaika huku mng’ao wa ngozi zao ukisahaulisha msongo wote wa mawazo.

Kwa madaha yote, muondoko wa “catwalk” (mwendo wa paka) uliotambulishwa na jinsi miguu yao ilivyopishana huku hatua zao zikikurudisha kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuvuta taswira vile Twiga hunyanyua miguu yake, huku tabasamu lililokolezwa na rangi za midomo zikikufikirisha uzuri wa maua ya mawaridi.

Hiyo yote, ni taswira ya tasnia ya ulimbwende wa mabinti wanaoiwakilisha Tanzania kwa urembo wao asilia kimataifa. Flaviana Matata, Miriam Odemba, Nancy Sumari na Herieth Paul ni miongoni mwa wanawake wa kupigiwa mfano katika tasnia hii.

Kwa mambo yote uliyoyafikiria, unaweza kuamini kama mwanafunzi anayesoma chuo kikuu akichukua masomo ya udaktari wa magonjwa ya binadamu au uhandisi anaweza kupata muda wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za mitindo ya mavazi?

Hiyo inawezekana kwa sababu kusoma masomo ya sayansi hakukunyimi fursa ya kushiriki shughuli nyingine za kijamii ambazo zinaweza kuwa na manufaa mengi kuliko kile unachosomea.

Sarafina Wasley na Elverenta Reuben, ni mabinti ambao wamejikita katika masomo ya udaktari na uhandisi ni miongoni mwa walimbwende wanaofanya vizuri katika tasnia sanaa Tanzania.

Kumekuwepo na dhana kuwa wanafunzi wa masomo haya ambayo wengi huyaona magumu kujihusisha na mambo ya sanaa hasa ambayo yanahitaji muda wa kufanya mazoezi na kujitunza kama muziki na hata ulimbwende. Ugumu huo haukuwasahaulisha mabinti hawa ndoto walizokuwa nazo tangu utoto wao.

Elverenta akitembea kwa madaha kwenye maonyesho ya mavazi ya mbunifu Ally Remtullah jijini Dar es Salaam. picha| Elverenta

Sarafina Wasley ambaye ni mhitimu wa udaktari wa magonjwa ya binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Habert Kairuki (HKMU) ambaye anasubiri mafunzo ya vitendo ili kutunukiwa udaktari wake. yeye alipenda kuvaa na kuonekana tangu akiwa mdogo.

Taswira ya haraka unaiweza kuipata jinsi gani binti mdogo hutembea pale avaapo nguo mpya lakini kwa Wasley mwenye miaka 25, haikuhitaji nguo mpya kupata munkari huo kwani kila vazi alilovaa, alijiona kama malkia ajaye.

Wakati Sarafina akianza safari yake na mavazi, Elverenta mara nyingi aligeuza sebule na korido za nyumba yao kuwa “run way” huku Baba yake akiwa shabiki namba moja aliyempigia makofi kila aliposhika kiuno na kutembea mithiri ya Nancy Sumari kwenye shindano la walimbwende wa dunia yaani Miss World.

“Ulimbwende ni kitu ambacho nimekuwa nikitamani kufanya tangu ningali mdogo na baba yangu alipenda kuniona nafanya hivyo. Aliweka wazi kuwa nacho ni kitu ninaweza kufanya na alinipatia baraka zote,” amesema  Elverenta, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) anayeingia mwaka wa nne akisomea uhandisi wa mazingira. 

Hadi sasa, mafanikio ambayo wamefikia warembo hawa ni pamoja na kushiriki mashindano mbalimbali ya ulimbwende likiwemo la Miss Universe 2019 kwa upande wa Tanzania ambapo wote waliingia kwenye tano bora ya mashindano hayo licha kuwa hawakuibuka washindi.

Mshindi wa kwanza alikuwa Shubila Stanton ambaye naye ni mwanafunzi wa chuo kikuu anyesomea sayansi ya mazingira.


“Kukatishwa tamaa kupo. Pale utakapokatishwa tamaa cha msingi ni kusimama na kuwaonyesha kwamba yote yanawezekana. Ninasoma na ninazingatia masomo yangu na bado ninaishi ndoto yangu,” – Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Elverenta Reuben.


Haikuwa rahisi kukubalika na jamii

Mabinti hawa ambao sanaa hii imewaunganisha kwa mwaka mmoja sasa tangu wakutane kwenye shughuli za ulimbwende, wamekuwa ni kama ndugu huku wakipitia changamoto mbalimbali kwenye tasnia hiyo.

Mbali na changamoto ya malipo madogo kuliko kazi wanazozifanya, changamoto zingine ni pamoja na mtazamo hasi kutoka kwa jamii ikiwa ni matokeo ya walimbwende wengine ambao hawakuwa mfano mzuri wa kuigwa kutokana na matendo yao.

Sarafina ameiambia www.nukta.co.tz  kuwa safari haikuwa rahisi pale wazazi wake walivyoingilia kati na kutaka kumzuia asiingie kwenye uanamitindo, ghasia za safari hiyo zilitulia pale alipowaeleza kuwa ni kitu anachopenda na hakitaathiri masomo yake.

Lakini ipo namna fulani ambayo wanachuo wenzake na hata wahadhiri wake walimtazama kana kwamba amepotea njia kusomea udaktari huku akipenda sanaa ya uanamitindo kwani wengi walihoji “uliona wapi daktari akicatwalk (akitembea mwendo wa paka)? muda huo anatoa wapi?” lakini hakuacha maneno ya watu yazuie ndoto zake.

Naye Elverenta anasema kama wakina mama wengine wa Afrika, mama yake siyo “mtu wa mchezo” sharti ambalo ameliweka kwenye kazi za mwanaye ni kupata taarifa ya kila hatua na kila kitu anachokifanya akiwa kwenye shughuli za uanamitinndo.

“Mama yangu siyo mtu wa mchezo. Lakini nilimwambia napenda na anajua kama akinizuia, nitafanya bila yeye kujua na hataki hilo. Ilimradi ninamwambia kila kitu, mama hana shida,” amesema Elverenta.

Sarafina Wasley(kulia) na Elveranta Reuben (kushoto) walipotembelea ofisi za nukta Africa Jijini dar es Salaam seedspace. Picha| \rodgers George

Matunda ya ndoto zao yameanza kuonekana

Harakati za vijana hawa wa kike ambao wameamua kuionyesha dunia kuwa wanaweza, zimewapunguzia wazazi wao majukumu ya kuwahudumia wakiwa masomoni kwani sanaa hiyo imeanza kuwapatia kipato cha kujikimu kimaisha licha ya kuwa siyo kikubwa ukilinganisha na kazi wanayofanya.

Wanadada hao ambao wana malengo makuba na sayansi wanayosomea, bado wanamalengo yenye ukubwa sawa kwenye sanaa wanayoifanya.

Katika kuzifanya ndoto zao kuwa za kweli, wameanza kufikiri namna ya kufanya kazi na makampuni ya kimataifa yanayojihusisha na mitindo ili wapate fursa ya kujifunza na kutembea katika maeneo mbalimbali duniani. 

Reuben ambaye sasa yupo masomoni, amesema kwa sasa anamalizia masomo ili angie kwenye sanaa hiyo kwa miguu miwili kwani ni ndoto yake ya muda mrefu.


Zinazohusiana


Pia wanaendelea kushambulia majukwaa ya Tanzania, ambapo Desemba mwaka huu wanatarajia kushiriki wiki ya mitindo ya mavazi ya Swahili Fashion Week endapo watakubaliwa, 

Warembo hao wameshavaa nguo za wabunifu wengi nchini akiwemo mbunifu Ally Remtullah.

Uzuri wa mabinti hawa ni ule wa kufanya kila jicho ligeuke kuwaangalia kwani ni Waafrika waliotaradadi uafrika wao na kwa matendo yao msemo wa “uzuri wenye akili” unatimia.

Endelea kusoma Nukta kwa simulizi za watu wengine na kufahamu zaidi biashara ya mitindo na ubunifu inavyoendeshwa Tanzania.

Enable Notifications OK No thanks