Makatibu mahsusi wenye umri mkubwa walalamika kubaguliwa kwa kigezo cha mvuto
- Ni kutokana na malalamiko ya kubaguliwa kuwa hawana mvuto.
- Uadilifu na weledi wasisitizwa.
Dar es salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewatia moyo makatibu mahsusi wenye umri mkubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maadili kwa sababu wanakumbuka vitu vingi vinavyohusu taasisi wanazofanyia kazi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo kwenye uzinduzi wa mkutano wa tisa wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo Juni 2, 2022 uliofanyika jijini Dodoma.
Kauli kiongozi huyo mkuu wa nchi imekuja mara baada ya Mwenyekiti wa TAPSEA Zuhura Maganga kusema miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo makatibu mahsusi wenye umri mkubwa ni kutopangiwa majukumu yao ya msingi kwa sababu ya kukosa mvuto.
“Aidha baadhi ya viongozi kuwa na tabia ya kupanga kazi kwa upendeleo hasa kwa makatibu mahsusi ambao umri wao umesogea kuonekana hawana mvuto kwa baadhi ya ofisi,” amesema Maganga huku akishangiliwa na makatibu mahsusi waliohudhuria hafla hiyo.
Hata hivyo, Rais Samia amesema wasivunjike moyo kwani kazi wananazozifanya ndizo zenye mvuto na maadili.
Amesema kuchafuliwa kwa sekta hiyo ya makatibu mahsusi kumetokana na baadhi ya waajiri kuajiri kwa kuzingatia mvuto badala ya weledi wa kazi na maadili.
“Masektetari ambao umri umekwenda kama wangu, kwa kweli ndiyo wachapa kazi, wala sitaki mvunjike moyo ndiyo wachapa kazi…kwa hiyo hawa tunaweza tukawa hatuna mvuto mzuri lakini akili zipo vizuri…kwa hiyo wazee wenzangu tuchape kazi,” amesema Rais na kushangiliwa na umati uliofurika ukumbini.
Soma zaidi:
Mkutano huo wa tisa wa makatibu mahsusi nchini unafanyika kwa siku mbili ukiwa na kau limbiu isemayo ‘Uwezo wa kitaaluma na ubunifu katika matumizi ya teknolojia unaimarisha maendeleo ya uchumi”
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TAPSEA, kaulimbiu hiyo ina lengo la kuhimiza ubunifu ambao ni chachu ya maendeleo kwani mtu akiwa mbunifu anafanya uzalishaji zaidi.
Samia sasa kuilea TAPSEA
Miongoni mwa jambo lililoibua shangwe na nderemo katika ukumbi wa Jakaya Kikwete ni mara baada ya Rais Samia kukubali ombi aliloombwa mwaka 2017 la kuwa mlezi wa chama hicho.
Rais Samia amesema amekubali kuwa mlezi wa chama hicho kutokana na kutambua changamoto ambazo makatibu mahsusi wanapitia sambamba na kuridhishwa na utendaji kazi wa viongozi wao ambao wamekuwa wakitii na kufuata maelekezo wanayopewa.
Pamoja na kukubali ombi hilo, Rais Samia amewaomba wanachama wa TAPSEA kuridhia uongozi uliopo ambao unatakiwa kuisha kesho Juni 3, 2022,tuendelee kuwepo madarakani kwani itakuwa rahisi kwake kushirikiana nao kwa ukaribu na kuongeza kuwa hakusudii kuingilia demokrasia yao hivyo wafikirie ombi hilo.
“Najua kila taasisi ina demokrasia, najua wakati wenu wa uchaguzi umefika lakini ili niweze kuilea vizuri taasisi hii nakuombeni mnipe muda, kwa sababu kwa majukumu yangu kuanza na watu wapya ni ngumu…..
“Nimesema naomba na hapa sikusudii kupinda demorasia yenu hapana ila nitafanya vizuri majukumu ya ulezi mkinipa watu wanaoijua, walioiendeleza taasisi hadi kufika hapa…. Kwa hiyo mkakae mlifikirie,” amesema Rais Samia.
Kwa sasa chama cha makatibu mahsusi Tanzania kina jumla ya wanachama 4,400 kutoka Tanzania bara na visiwani ambao wanafanya kazi katika taasisi mbalimbali ambazo zipo chini ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Pamoja na mambo mengine wamesisitizwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia weledi na uadilifu pamoja na kutunza siri za taasisi wanazofanyia kazi.
Latest
