Majaliwa aishawishi Toshiba kuwekeza Tanzania

August 27, 2019 3:13 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ameiomba kampuni ya Toshiba ya nchini Japan ifungue ofisi na kuwekeza katika viwanda nchini Tanzania.
  • Amesema Serikali imeweka mazingira mazuri na soko la bidhaa watakazotengeneza lipo ndani na nje ya nchi. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Toshiba nchini Japan na kuwashawishi kuwekeza katika viwanda vya bidhaa za elektroniki Tanzania. 

Toshiba hutengeneza vifaa vya kielektroniki na mitambo zikiwemo kompyuta na majenereta. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Agosti 27, 2019) baada ya kutembelea Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya Toshiba na kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na kampuni hiyo.

 Majaliwa ameishawishi Toshiba kuwekeza Tanzania na ifungue viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki kama vile redio, televisheni, pasi na viwanda vingine watakavyoona wao vinafaa kujengwa nchini.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amewahakikisha viongozi hao kwamba hawatojuta kuwekeza Tanzania kutokana na sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara pamoja na soko la uhakika wa bidhaa zitakazozalishwa kwa kuwa Tanzania imezungukwa na nchi nyingi.

 “Wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza Tanzania wakiwemo na wa kutoka Japan pamoja na kampuni ya Toshiba, watambue kwamba Serikali ya awamu ya tano imeboresha mazingira ya uwekezaji na kuyafanya yawe rafiki, nina uhakika wawekezaji watakaoamua kuwekeza Tanzania hawatajutia uamuzi wao huo,” amesema Majaliwa katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na ofisi yake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa kiwanda cha kutengeneza mitambo ya  kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na kampuni ya Toshiba nchini Japan wakati alipotembelea kiwanda hicho, Agosti 27, 2019. Kushoto ni Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Japan, John Kambona.  Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sayansi ya Toshiba, Takano Lwakiri amemwambia Majaliwa kuwa kampuni yake iko tayari kupanua ofisi yake ya Tanzania na kufungua biashara, ambapo ameomba yafanyike mazungumzo yatakayotoa dira sahihi ya kufanikisha jambo hilo.

Iwapo Toshiba watawekeza Tanzania kama walivyoahidi wito huo, ujio wa kampuni hiyo kubwa kutoka Japan utawapa Watanzania fursa ya kujifunza teknolojia mpya, ajira na namna bora ya uendeshaji wa biashara unaozingatia viwango vya  kimataifa.

Toshiba, yenye umri wa miaka zaidi 144,  hadi hadi Machi 2019 ilikuwa na wafanyakazi 128,697 huku ikiwa na kampuni tanzu 350 na nyingine 120 zinazohusiana nazo.

Mapema Mei mwaka huu kampuni hiyo ilifungua tawi nchini Kenya ili kuongeza wigo wa uwekezaji wake.


Zinazohusiana: 


Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema anaamini Mkutano wa Saba wa “Tokyo International Conference on Africa Development” (TICAD 7) utakaoanza kesho Yokohama, Japan  utakuwa na mafanikio makubwa kutokana na ajenda zilizoandaliwa.

Miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na namna ya kuunganisha shughuli za biashara baina ya Serikali na sekta binafsi.

Amesema kwa kutumia mkutano huo wa TICAD 7 wafanyabiashara wa Tanzania wanayo fursa ya kunufaika kwa kuunganisha nguvu zao na makampuni makubwa ya Japan kama Toshiba ili kupata uzoefu na teknolojia muafaka. 

 Waziri Mkuu yuko nchini Japan akimwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano wa TICAD 7 utakaoanza kesho, ambapo ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi wengine wa Serikali na taasisi za Umma.

Enable Notifications OK No thanks