Magari maarufu zaidi nchini Tanzania

March 15, 2022 8:58 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Orodha ya 10 bora imetolewa na kampuni ya SBT ya nchini Japan inayoingiza magari yaliyotumika nchini Tanzania.
  • Asilimia 70 ya orodha hiyo imetawaliwa na gari za kampuni  ya Toyota.
  • Gharama za manunuzi, upatikanaji wa spea ni kati ya sababu ya gari hizi kuagizwa zaidi.

Dar es Salaam. Ni kweli kila mtu anasafiri kwa uwezo wa pochi yake.  Na ni pochi hiy hiyo inayosababisha utofauti wa magari ambayo Watanzania wanapendelea kununua zaidi.

Kama mdau wa usafiri, ni wazi kuwa yapo magari ambayo huwezi hauwezi kumaliza siku bila kuyaona barabarani. Hiyo ni kutokana na sifa za magari hayo ikiwemo uwezo wake wa kuhimili changamoto za barabara za vumbi.

Sifa na nyingine, zimekuwa zikiwavutia Watanzania kununua baadhi ya magari zaidi kuliko mengine.

Mdau wa usafiri huo kutoka jijini Dar es Salaam, Peter Mashauri ameiambia Nukta Habari kuwa, watu hununua magari kwa kuzingatia maeneo wanayoishi, gharama za kutunza gari hilo, upatikanaji wa spea na  matumizi.

“Kwa mtu mwenye uwezo kiuchumi, atanunua gari kubwa mfano V8, Range na mengineyo lakini mtu huyo huyo anaweza kutaka gari kwa ajiri ya biashara (uber na bolt) akanunua IST maana ndiyo zinafahamika zaidi,” amesema Mashauri.

Kampuni ya kuagiza magari nchini Japan ya SBT imetoa orodha ya magari ambayo kutokana na kuagizwa kwake, yametambulika kama magari maarufu zaidi nchini Tanzania.

Hii ndiyo orodha ya magari 10 yanayotumiwa zaidi na Watanzania:

09. Toyota Raum

Gari hii haikuwepo kwenye orodha iliyotoka mwaka jana. Katika kipindi hicho, nafasi hii ilikuwa imechukuliwa na Toyota Corolla Lumion.

Kwa mujibu wa makadirio ya SBT, gari hii inagharimu kuanzia Sh6.1 milioni (bila kodi) ikiwa imeshatembea umbali wa kilometa 133,000. Kwa gari zilizotembea umbali mfupi, gharama yake ni ya juu zaidi.

Pia, gharama zinatofautiana kulingana na muundo wa gari na umbali ambao gari hiyo imetumika kabla ya kuingia Tanzania.

Sifa kuu za gari hiyo ni uwezo wa injini ya cc1490, siti tano, milango mitano na uwezo wa kuendeshwa matairi mawili au manne.

Sifa kuu za gari hiyo ni uwezo wa injini ya cc1490. Picha| Wikipedia.

08. Nissan Dualis

Gari hii pia ni mpya kwenye orodha ya SBT kwani mwaka jana, nafasi hii ilikuwa ni ya Toyota Ractis. 

Sifa kubwa ya Dualis ni ukubwa wa gari na starehe kwa mtumiaji wake. Mmoja wa watumiaji wa gari hiyo amesema uzuri wa gari hiyo ni uwezo wa kutulia barabarani na upatikanaji mzuri wa spea.

Gari hii inapatikana kwa gharama kuanzia Sh10.2 milioni, bei ya gari iliyotembea umbali wa  kilometa 233,000. 

07. Subaru Forester

Gari hii imeng’ang’ania kwenye nafasi hii kwani ilikuwa hapa hapa mwaka jana.

Forester inapatikana kuanzia Sh7 milioni, bei hiyo ni kwa gari ambayo imetembea kwa kilometa 220,000. 

Sifa kubwa ya gari hii ni siti tano na uwezo wa injini yake ni cc1,994. Usisahau kuwa gharama za kodi hazihusiki kwenye bei hizo.

06. Toyota Harrier

Kasi ya kuagiza magari haya imepungua kwani mwaka jana, Harrier ilikuwa imeshika nafasi ya tatu.

Ndinga hii injini yake ina uwezo wa kuanzia cc1,986 hadi cc3,456. Inasifika kwa kuinuka na uwezo wake wa kupita kwenye kila aina ya barabara. Zaidi, uimara. 

Unaweza pata chombo hii kwa gharama ya kuanzia Sh16 milioni ikiwa imetembelea kwa umbali kuanzia kilometa 176,000.


Soma zaidi


05. Toyota Premio

Inamuonekano fulani hivi wa kuvutia na imeshikilia nafasi hii tangu mwaka jana.

Premio ambayo bei yake ya chini ya kuagizia ni Sh8.7 milioni in uwezo wa injini yake ni cc1,496 hadi cc1,998. Wadau wa Nukta wamesema wale wote waliopenda Toyota Sprinter na matoleo ya kale ya aina ya gari za Saloon, wataifurahia hii pia.

04. Toyota Crown

Mwaka jana ilikuwa imeshika nafasi ya pili lakini kwa orodha ya mwaka huu, watu huenda hawajaiagizia sana.

Gari hiyo inaagizwa kwa kima cha chini cha Sh7.7 milioni bila kuhusisha kodi huku muonekano wake wa ndani unaweza kukusahaulisha shida za dunia.

Crown ambayo wamiliki wake hujiita “Royalty” yaani wanafamilia wa ukoo wa kifalme ina injini yenye uwezo wa cc1,988 hadi  cc2,997.

03. Toyota Corolla Rumion

Gari hizi zimeagizwa sana mwaka 2020/21 kwani mwaka jana, gari hii ilikuwa nafasi ya tisa.

Rumion uwezo wa injini yake ni cc1,496 hadi cc1,797 inaagizwa kwa bei ya kuanzia Sh9 milioni bila kodi. 

Rumion uwezo wa injini yake ni cc1,496 hadi cc1,797. Picha| Wikimedia.

02. Toyota Alphard

Ndinga hii imejizolea umaarufu miongoni mwa Watanzania kwani imeagizwa zaidi ikilinganishwa na mwaka 2020/21 ambapo ilishika nafasi ya nne.

Huenda uwezo wa injini yake ambao ni cc2,362 hadi cc3,456 pamoja na kufaa kwa matumizi ya familia na ofisi ikawa ni sababu ya gari hili kupendwa sana.

Gari hii yenye muonekano wa kifahari wa aina ya gari za “mini van” inaanzia gharama ya Sh9 milioni na kuendelea.

01. Toyota IST

Huenda ulitegemea kwa gari hii kuwa hapa kwani tangu nianze kuandika makala za magari mwaka 2019, gari hii haijawahi kung’olewa hapa.

Sifa yake ya kutumia mafuta kiasi, gharama nafuu ya manunuzi na ufahari wa udogo wake imefanya gari hizi kutumika sana nchini hasa kwa biashara ya usafiri na kwa baadhi ya watu gari hizi zimekuwa usafiri wa kuanzia maisha.

Gari hiyo ina uwezo wa injini kuanzia cc1,298 hadi cc1,797 inaweza kuagizwa kwa Sh6.7 milioni kama bei ya chini zaidi kwenye tovuti ya SBT. Bei hiyo haijajumuisha kodi na gharama za bima hivyo kabla ya kutaka kununua, ni vyema ukajifanya utafiti wako.

Tukutane mwakani mdau, huenda IST ikang’olewa lakini kuna gari kama Spacio, Ractis ambazo zilikuwa kwenye nafasi nzuri mwaka jana lakini mwaka huu hazipo.

Enable Notifications OK No thanks