Tanzania kujenga kituo cha upandikizaji figo kikubwa zaidi Afrika
- Kinatarajiwa kuwa kituo kikubwa katika Ukanda wa Jangwa la Sahala
- Pia kituo hicho kitatumika katika kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa kituo kikubwa cha kupandikiza figo pamoja, hatua inayoboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi nchini na Afrika.
Kituo hicho kinachotarajiwa kujengwa ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, pia kitakua kinatoa mafunzo kwa madaktari bingwa ili kuongeza wataalamu katika fani hiyo.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya mradi huo Mei 26, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Westin, jijini Osaka, Japan ambapo mradi huo unakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh28 bilioni.
Waziri mkuu Majaliwa aliondoka nchini kuelekea Japan kumuwakilisha Rais Samia kwenye maonyesho ya World Expo Osaka 2025.
Mradi huo unaofadhiriwa kama msaada wa moja kwa moja usio na masharti kutoka kwa wadau wa Japan utajengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Tiba la TOKUSHUKAI la Japan, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema kuwa makubaliano hayo yanahusisha ujenzi wa kituo cha umahiri kwa ajili ya huduma za upandikizaji figo na mafunzo ya kitabibu.
“MOU hii ambayo tumeisaini sasa hivi (jana Mei 26, 2025) ni kwa ajili ya kujenga kituo cha umahiri katika upandikizaji figo kwenye eneo la Tanzania na Ukanda wa Jangwa la Sahara,” amesema Profesa Makubi.

Profesa Makubi amesema ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kuanza mwaka huu na kukamilika ndani ya miaka mitatu, ambapo Serikali ya Tanzania imepanga kusaidia katika baadhi ya maeneo kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa mafanikio.
“Kituo hiki hakitahudumia Watanzania pekee, bali pia wananchi kutoka mataifa mengine ya Afrika, na kitatumika pia kwa ajili ya kufanya tafiti na kutoa mafunzo ya kitabibu ya figo,” amesema Profesa Makubi.
Hadi kufikia Januari 2024, Tanzania ilikuwa na vituo vya afya 59 vikiwemo 29 vya umma zinavyotoa huduma saidizi za kuchuja damu (dialysis) kupitia mashine 649 za kusafisha damu.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lugano Kusiluka amesema UDOM itaendelea kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa katika kutoa mafunzo kwa wataalam wa upandikizaji figo pamoja na kutekeleza tafiti za kitabibu.
“Kwa sasa tupo kwenye hatua za awali za kuanzisha programu ya uhandisi wa vifaa tiba, ili kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo ya vifaa tiba,” amesema Profesa Kusiluka.

Faida nyingine za kituo hicho
Profesa Kusiluka amesema kituo hicho kitawezesha pia kufundisha na kutunza vifaa tiba kwa usahihi, na kusaidia juhudi za kitaifa za kupunguza gharama za matibabu ya figo na kuimarisha huduma bora za kiafya.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya za Januari 2024, Tanzania hutumia kati ya Sh88.1 bilioni na Sh110.2 kila mwaka kwa wagonjwa wasio na uwezo kupata tiba ya kuchuja damu kwa utaratibu wa msamaha.
Latest



