CCM yaahidi kutengeneza ajira milioni 8 ifikapo 2030

May 30, 2025 7:40 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaja na vipaumbele nane vya kimkakati.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimezindua ilani mpya ya uchaguzi kwa mwaka 2025-30 yenye vipaumbele nane ambavyo vimelenga kutatua baadhi ya changamoto lukuki zinazowakabili Watanzania zikiwemo ukosefu wa ajira, ongezeko la gharama za maisha na mahitaji makubwa ya miundombinu hususan barabara. 

Ilani hiyo, iwapo CCM itashinda uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, itakuwa ni muongozo wa Serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano. 

Kipaumbele cha kwanza cha ilani ya CCM ya 2025 ni kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa kuongeza thamani rasilimali zinazozalishwa nchini.

Ili kutekeleza hayo, CCM imepanga kuimarisha ukuaji jumuishi wa uchumi, kuimarisha sekta binafsi, kuimarisha na kukuza sekta za kimageuzi za uzalishaji, kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuimarisha matumizi endelevu ya ardhi. 

Mipango mingine ya chama hicho tawala ni kukuza utalii, kuimarisha mchango wa uchumi wa buluu katika kukuza Uchumi wa Taifa na kuimarisha uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Katika ilani ya mwaka 2020 CCM ililenga kuhakikisha uchumi wa Taifa unakua kwa wastani wa asilimia 8 kila mwaka, lengo ambalo bado halijafikiwa likiathiriwa zaidi na ikiwemo janga la Uviko- 19 na mfumuko wa bei uliochochewa na migogoro ya kimataifa. 

Ripoti za uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinabainisha kuwa mwaka 2024 uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya mwisho ya mwaka.

Yaongeza ahadi ya ajira

CCM imeendelea kuahidi kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umaskini huku ikibakiza lengo la kuzalisha ajira zisizopungua milioni 8 ifikapo mwaka 2030 kutoka katika sekta rasmi na zisio rasmi. 

“CCM inalenga kuona kuwa nusu ya ajira hizo zinazalishwa katika sekta rasmi,”Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya mwaka 2025, Prof Kitila Mkumbo amewaambia wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM jijini Dodoma. 

Chama hicho kimeongeza lengo la kuzalisha ajira kwa kuongeza lengo la ajira zaidi ya milioni 1 kutoka ajira zisizopungua milioni 7 zilizobainishwa katika ilani ya mwaka 2020 inayotamatika mwaka huu. 

Ahadi hiyo inakuja katika kipindi ambacho kuna tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kutokana na idadi ya vijana wanaohitimu vyuo vya kati na vyuo vikuu kuwa kubwa kuliko kasi ya uzalishaji wa ajira nchini kutoka sekta rasmi na isiyo rasmi.

Miezi miwili iliyopita Serikali iliunda timu ya wataalamu kushughulikia changamoto za Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira Tanzania  (Neto) kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2023.

Prof Kitila amesema chama hicho kitaisimamia Serikali kuhakikisha inakuza na kuwezesha shughuli za kiuchumi zinazoanzishwa na kuendeshwa na Watanzania ili kuwapa fursa ya kuendelea kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Uboreshaji wa huduma za jamii 

Katika kipaumbele chake cha tatu, CCM imepanga kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii kupitia upatikanaji wa huduma bora za jamii kwa wote ikiwemo elimu, afya, maji, umeme, hifadhi ya jamii, na makazi bora.

“Katika miaka mitano ijayo, CCM itaendelea kuzisimamia Serikali kuendelea kuwekeza katika kupanua huduma bora za jamii na kuweka mifumo thabiti ya ugharimiaji wa huduma hizo engo ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za jamii na kwa gharama nafuu,” inabainisha ilani ya CCM.

Vipaumbele vingine viinavyokusudiwa kutekelezwa na Ilani ya CCM ni pamoja na Kuimarisha Miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii, pamoja na kudumisha demokrasia na utawala bora.

Aidha, vipaumbele vya mwisho ni kudumisha muungano, amani, utulivu, usalama na diplomasia ya kimataifa pamoja na kudumisha utamaduni wa Taifa na kukuza sanaa na michezo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema ilani mpya ya chama hicho ya mwaka 2025- 2030 inatekelezeka kutokana na mipango na uwezo wa Serikali yake.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza mara baada ya uzinduzi wa ilani hiyo leo Mei 30, 2025 jijini Dodoma amesema ili chama chake kiweze kutekeleza yaliyoahidiwa ni kuweka utulivu ndani ya nchi, kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na sekta binafsi ya ndani na ya nje. 

Rais Samia amezindua ilani hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ambao yeye mwenyewe anatarajia kugombea katika nafasi ya Urais  ili kutetea nafasi aliyonayo kwa miaka mingine mitano. 

Kwa miaka mitano iliyopita, CCM kupitia serikali yake imekuwa ikitekeleza ilani  kwa kauli mbiu ya “Tumetekeleza kwa Kishindo, Tunasonga Mbele Pamoja”, ikiahidi kuimarisha uchumi, kutengeneza ajira, kuboresha huduma za kijamii, na kuijenga Tanzania ya viwanda.

Kwa mujibu wa Rais Samia maudhui ya ilani mpya ya 2025 yamezingatia maoni na matarajio ya wanachama wa CCM, wananchi na wadau mbalimbali walioshiriki kutoa maoni yao kuhusu mambo ya kuzingatiwa katika ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks