Maeneo sita muhimu ya kutupia macho mwelekeo wa Serikali 2024

January 4, 2024 10:56 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuanza kwa safari za SGR Dar es Salaam – Dodoma ifikapo Julai 2024 na kuwashwa kwa mitambo ya (JNHPP).
  • Kunategemewa kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea uzalishaji, jambo litakalokuza uchumi.

Dar es Salaam. Disemba 31, 2023 Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alihutubia Taifa, akitoa mwelekeo wa Serikali yake kwa mwaka 2024 ambapo aliainisha baadhi ya matukio muhimu ya kutupiwa macho katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Hotuba hiyo ni ya pili kwa Rais Samia tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 alipochukua kiti cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021.

Nukta Habari tumekuandalia uchambuzi wa kina wa maeneo muhimu yanayopaswa kutupiwa macho na Watanzania, kwa kuwa kwa kiasi kikubwa yanagusa mustakabali wa maisha yao kwa namna tofauti.


Soma zaidi:Umemejua unavyowaokoa wafugaji na ukame Dodoma


Kuanza kwa safari za (SGR) Dar-Dodoma ifikapo Julai 2024

Tangu kuanza kwake mwaka 2017 mradi wa reli ya kisasa (SGR) ni miongoni mwa miradi iliyotupiwa macho zaidi na Watanzania wakiwa na  matarajio ya kuwapunguzia adha ya usafiri kwa kupunguza muda unaotumika wakati wa safari.

Licha ya umuhimu wake kiuchumi,  mradi huo umekuwa ukisuasua kwa miaka mitano mfululizo tangu kuanza kwa utekelezaji wake jambo lililo mfanya Rais Samia kutoa maagizo kwa wahusika kuhakikisha moaka ifikapo Julai 2024, safari za SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma ziwe zimeanza.

“Nimekuwa nikisikia mabadiliko ya tarehe za kuanza kwa safari za treni na kwa kweli, wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi. Sasa, naelekeza ifikapo mwisho mwa Julai 2024, safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma zianze,” alisema Rais Samia.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu kabisa wa nchi kutoa agizo hilo lililofuata baada ya ahadi za viongozi nane wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kuanza kwa safari za SGR kunatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwa muingiliano wa watu utaongezeka, pamoja na kupungua kwa muda wa kusafiri kwa magari.

Sehemu ya kichwa cha treni ya kisasa ya SGR wakati kikiwasili katika bandari ya Dar es Salaam.Picha|TRC

Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP)

Mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Rufiji mkoani Pwani ulianza mwaka 2017 ukitarajiwa kuzalisha Megawati 2,115 zitazoingizwa kwenye gridi ya Taifa na kumaliza changamoto ya mgao wa umeme unaoendelea nchini huvi sasa ambao umekuwa kero kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Rais Samia kinu cha kwanza cha kufua umeme kinatarajiwa kuwashwa rasmi Februari  2024, huku kinu cha pili kikitarajiwa kuwashwa mwezi Machi 2024 hatua inayotegemewa  kuzalisha Megawati 470.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, mahitaji ya umeme nchini yameongezeka kutoka Megawati 1,276 iliyokuwepo mwaka 2021/2022 hadi 1,363 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 6.9.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kumaliza tatizo la mgao wa umeme na kuimarisha zaidi shughuli za kiuchumi ikiwemo viwanda kama anavyofafanua Mhadhiri wa Chuo cha Mzumbe na mchambuzi wa masuala ya uchumi Dk Romanus Dimoso.

“Kuwashwa kwa hiyo mitambo kutasaidia kukua kwa shughuli mbalimbali za uchumi…hata hivyo hii haitoshi tunahitaji uzalishaji wa umeme zaidi ili tuweze kuuza na nchi jirani,” amesema.

Aidha, Dk. Dimoso ameitaka Serikali kutokuchelewa kuwasha mitambo hiyo ikiwa hatua zote za utengenezaji zimekamilika kwa kuwa  kunaweza kusababisha mitambo hiyo kuharibika kwa kutu na kuliingiza Taifa gharama ya ukarabati. 


Soma zaidi:Elimu ya Veta inavyowainua walemavu wa akili Tanzania


Kuimarishwa kwa vitengo vya maafa na uokozi

Licha ya kuwa na miongo saba tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania, bado kumekuwepo na vilio vya watanzania juu ya kukosa huduma za jeshi hilo pale inapotatikana.

Kutofika eneo la kutoa msaada kwa wakati, vifaa hafifu vya kufanyia kazi na uhaba wa watumishi ni miongoni mwa sababu zinazolalamikiwa mara kwa mara na wananchi kuwa ndio zinazokwamisha jeshi hilo kutekeleza majukumu muhimu ya kuokoa raia na mali zao katika majanga mbalimbali ikiwemo moto.

Mathalani majanga mfululizo yaliyotokea nchini Tanzania ikiwemo ajali ya ndege ya Precision Air, kuungua kwa soko la Kariakoo, pamoja na mafuriko ya matope hanang ni mfano tosha wa namna gani Tanzania inatakiwa kujidhatiti kwa kuwa na vifaa bora pamoja na rasilimali watu ya kutosha kwa ajili ya uokozi.

Huenda hiyo ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Rais Samia kuliingiza jeshi hilo katika orodha ya taasisi zitakazoimarishwa mwaka 2024 ikiwemo kitengo cha maafa kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Elimu 

2023 ni miongoni mwa miaka muhimu kwa wadau wa elimu nchini, mara baada ya Serikali kuridhia na kupitisha mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 yanayolenga kuimarisha utolewaji wa elimu kuendana na mahitaji ya sasa.

Mabadiliko hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  yatatekelezwa kwa awamu ambapo madarasa yatakayoanza na mitaala mipya ni awali, la kwanza na la tatu kwa shule za msingi na kidato cha kwanza shule za mkondo wa amali (ufundi stadi) pekee.

Kwa mujibu wa Waziri wa wizara hiyo, Prof Adolf Mkenda, Sera hiyo itawawezesha  wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kupata vyeti viwili ambavyo ni cha elimu ya sekondari na ufundi (Amali) jambo litakalochangia kuongeza wataalamu katika fani mbalimbali nchini.

Nukta habari imezungumza na mdau wa elimu nchini Tanzania Richard Mabala, ambaye amebainisha kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuleta matokeo chanya ikiwa Serikali itawaruhusu wanafunzi kuwa na uwanja mpana wa kuchagua aina ya mafunzo kulinganana uhitaji wao.

“Nimeambiwa kwamba kila shule itachagua vipaji viwili ikiwa hivyo shule yako ikichagua kipaji ambacho siyo cha kwako utafanyaje? Inawezeana kuna shule zitakuwa na vipaji vingi na nyingine ambazo zitakuwa na vipaji vichache,” amesema Mabala.

Aidha, Mabala ameitaka Serikali kuongeza muda wa kufundisha kwa walimu kuhusu mtaala huo ili kuwawezesha kuwa  mahiri katika kutoa mafunzo na kutunga mitihani itakayoendana na mafunzo hayo.

Rais wa  Samia Suluhu Hassan(katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania Startup Association (TSA).Picha|Ikulu

Kustawisha Kampuni changa (startups)

Ikiwa wewe ni mwanzilishi wa kampuni changa au startups mwaka 2024 usikae kinyonge kwani Serikali imedhamiria kuweka mazingira wezeshi ili kustawisha kampuni hizo zenye mchango katika ukuaji wa uchumi.

Kwa miaka miwili mfululizo Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka mazingira wezeshi kuboresha kampuni hizo ikiwemo ahadi ya kuweka sera wezeshi za startups ambapo Rais Samia aliahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa (start- ups) ili zikue.

“Umuhimu wa kampuni changa umeendelea kukua nchini, Serikali itaendela kushirikiana zaidi na taasisi tanzu za kampuni changa na kuendelea  kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wake, amesema Rais Samia,” amesema Rais Samia.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

Miongoni mwa mambo yanayotupiwa macho na Watanzania wengi ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utaofanyika 2024 ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Uchaguzi huo hulenga kupata viongozi wa Serikali za Mitaa ngazi ya vijiji ikiwa ndio ngazi ya chini zaidi inayotegemewa kupenyeza ajenda mbalimbali za kitaifa ikiwemo uchaguzi mkuu wa Urais, wabunge na madiwani watakaoiongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.

Katika hotuba yake Rais Samia amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kuwa kutawapa nafasi ya kuwachagua viongozi wanaofaa.

Rais Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka Watanzania kuazimia kubadilika kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu ili mwaka 2024 uwe wa utekelezaji na matokeo zaidi.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV