Tanzania yazindua reli ya SGR kuchochea mapinduzi ya uchumi
- Rais Samia ataka iendeshwe kibiashara ili kupata tija iliyokusudiwa haraka.
- Inatarajiwa kufungua fursa za ajira, kuongeza ufanisi wa bandari pamoja na ongezeko la biashara kitaifa na kimataifa.
Dar es Salaam. Tanzania imezindua rasmi safari za treni katika reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma huku Rais Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa mradi huo utachochea mapinduzi makubwa ya kiuchumi.
Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa uendeshaji wa reli hiyo jijini Dodoma leo, Rais Samia amesema mradi huo utafungua fursa za ajira, kuongeza ufanisi wa bandari pamoja na ongezeko la biashara kitaifa na kimataifa.
Ndani ya kipindi cha miaka 10, Tanzania imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miradi mikubwa ya miundombinu ya uchukuzi na nishati ukiwemo ujenzi wa mtandao wa kilomita 1,219 wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere linalozalisha Megawati 2,115.
Sehemu kubwa ya uwekezaji huo umelenga kukuza uchumi kupitia ongezeko la biashara ndani ya nchi na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ule wa ukanda wa kusini.
Rais Samia amewaambia baadhi ya wakazi wa Dodoma waliojitokeza katika hafla hiyo kuwa reli hiyo inatoa fursa kwa wafanyabiashara, kuchochea shughuli za kiuchumi kwenye viwanda, kilimo, uvuvi pamoja na utalii.
“Zaidi tunatarajia reli hii itaongeza ufanisi wa bandari zetu hususan bandari ya Dar es Salaam kwa kuondosha mizigo kwa haraka kutokana uwezo mkubwa wa reli hii kuhudumia shehena ya tani 17 milioni kwa mwaka,” amesema Rais Samia.
Huduma za usafiri zilizozinduliwa rasmi leo zitatumia vipande viwili vya awali vya mradi huo vyenye urefu wa kilomita 722 zikiwemo njia kuu na mapishano ikiwa ni sehemu ya mtandao wa kilomita 1,219 hadi jijini Mwanza.
Malengo ya Tanzania, kwa mujibu wa Rais Samia ni kuendeleza kujenga reli hiyo kuongeza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani hususan zisizo na bandari zinazohudumiwa na Ushoroba wa Kati yaani Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Uganda na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi.
Rais Samia amezindua rasmi safari za SGR leo ikiwa imepita miezi saba tangu atoe agizo hilo kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Disemba 31, 2023 kuanza safari zake ifikapo Julai mwaka huu.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza safari za SGR zilianza rasmi Juni 14, 2024 kwa safari kati ya Dar es Salaam mpaka Morogoro na kisha Julai 25, 2024 safari kati ya Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma zilianza ikiwa zimesalia siku nne tu kabla ya muda aliotangaza Rais kuisha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa tangu kuanza kwa safari za SGR mpaka Julai 28, 2024 jumla ya abiria 188,000 wametumia usafiri huo uliogharimu Dola za Marekani Bilioni 3.138 sawa Sh7.84 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya SGR kwa vipande viwili vya Dar es Salaam- Morogoro na Morogoro – Makutupora mkoani Dodoma.
Mpaka sasa kwa mujibu wa Kadogosa mtandao huo wa reli umegharibu Dola za Marekani bilioni 10 za Marekani sawa na Sh 20.3 trilioni ambapo Rais Samia amesema anatamani gharama hizo zisalie hivyo kwa kuwa ni fedha nyingi.
“Nami nami namuomba Mungu hizo gharama zisiongezeke ibaki hivyo hivyo, maana likitokea lolote gharama zikaongezeka itakuwa ni kazi kwa upande wetu, fedha hizi ni nyingi sana hivyo tuna wajibu wa kuulinda na kuutunza mradi huu,” amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa safari za SGR jijini Dodoma. Picha l Ikulu.
SGR kuathiri mabasi, malori
Pamoja na athari chanya zinazotarajiwa kutokana na SGR, upo wasiwasi kwamba wafanyabiashara wa mabasi na malori hususan katika maeneo yenye SGR wakaathirika.
Kwa mujibu wa Kadogosa treni ya abiria ina uwezo wa kusafirisha watu 6,000 kwa siku moja, sawa na mabasi 100 ya abiria 60.
Kwa upande wa treni ya mizigo, Kadogosa alibainisha kuwa treni hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 za mizigo sawa na magari 500 yenye uwezo wa kubeba tani 20 kwa kila moja.
Hata hivyo, Rais Samia amesema kupungua kwa abiria katika maeneo yenye treni ya SGR ni fursa kwa wafanyabiashara wa malori na mabasi kutizama maeneo mengine yenye uhaba wa huduma hiyo ya usafiri.
“Ninajua kuwepo kwa mradi huu mdogo wangu Abood (Mmiliki wa mabasi ya Abood na Mbunge wa Morogoro Mjini Abdulaziz M. Abood) utaumia kidogo… nataarifa niliyonayo kashapunguza mabasi barabarani lakini Tanzania hii ni kubwa chukua mabasi peleka sehemu nyingine tutakusaidia,” amebainisha Rais Samia wakati akiongea na wakazi wa Morogoro alipokuwa safarini kutokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Serikali ya Rais Samia inaendelea kujenga mradi huo katika kipindi ambacho inakabiriwa na mahitaji makubwa ya kifedha kutokana na shinikizo la kuongezeka kwa deni la Serikali na ukuaji wa taratibu wa mapato ya kikodi ambayo hayatoshelezi kugharamia miradi hiyo mikubwa.
Mwaka 2020 Tanzania ilikopa Dola za Marekani bilioni 1.46 sawa na Sh 4.320 trilioni za Tanzania kutoka kwa Benki ya Standard Chartered kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa kilomita 550 za reli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
SGR iendeshwe kimkakati
Rais Samia ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Bodi ya TRC kuweka mikakati ya kuendesha SGR kibiashara ili tija iliyokusudiwa ipatikane haraka akisisitiza haitakuwa vyema Serikali kuendelea kulipa deni ililokopa kujenga reli hiyo huku yenyewe ikiendeshwa kwa hasara.
“Ingependeza sana shirika likafanya kazi kwa faida na likachangia kulipa deni tulilokopa, nikutake msajili wa hazina ukae na bodi na menejimenti ya TRC muweke vigezo vya utendaji wa kazi (KPI) na mzifuatilie kwa ukaribu zaidi,” amesema Rais Samia.
Latest