Elimu ya Veta inavyowainua walemavu wa akili Tanzania
- Baadhi wamehitimu na kuwa walimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
- Jamii yatakiwa kuendelea kushirikiana na walemavu na kuwapenda.
- Walimu washauriwa kuwa wabunifu ili kupata matokeo chanya.
Dar es Salaam. Awali, ilikuwa ni vigumu kushuhudia watu wanaozaliwa na ulemavu wakipata huduma muhimu wanazozihitaji kama elimu, afya, pamoja na kushirikiana na wanajamii wengine kuibua suluhu za matatizo yanayozikabili jamii zao.
Hivi sasa zama hizo zimepita. Kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali pamoja na wadau, ikiwemo kuielimisha jamii kutowabagua na kushirikiana na kundi hilo, kama binadamu wengine watu wenye ulemavu nao wanapata huduma wanazostahili.
Miongoni mwao ni kijana Paulo Ngunyali, mhitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Chang’ombe, Jijini Dar es Salaam. Pamoja kuwa mlemavu wa akili amehitimu fani ya uundaji wa mashine, na sasa ni mwalimu msaidizi katika kitengo cha watu wenye mahitaji maalumu.
Katika maonesho ya kimataifa ya kibiashara maarufu kama Saba Saba, Paulo (32), amekuwa kivutio cha wengi kutokana na namna anavyoelezea kwa ufasaha jinsi mashine ya kupima uwezo wa kufundishaa watu wenye ulemavu wa akili inavyofanya kazi.
“Anapokuja mwanafunzi mwa mara ya kwanza, badala ya kumwambia aandike sisi tutamleta hapa atakichezea hiki chombo kwa muda mfupi kisha tutajua kuwa anafundishika au hafundishiki,” anaeleza Paulo.
Mashine maalumu ya kupimia uwezo wa kufundishika mwa mtu mwenye ulemavu wa akili.PichalEsau Ng’umbi/Nukta
Mwanafunzi anayepimwa uelewa kupitia mashine hiyo atatakiwa kufuatisha michoro iliyopo kwenye kibao kwa kutumia kalamu maalumu ambapo kalamu hiyo ikigusana na kibao hutoa mlio fulani utakaomchochea mhusika kuendelea kufuatisha michoro iliyopo mpaka atakapomaliza.
“Baada ya hapo nitamtaka aweke kalamu katika vitundu vilivyopo kwenye kibao hiki, hapa kuna matundu ya kweli na bandia, hivyo tunapima uwezo wake wa kufikiri kwa kuangalia iwapo atatambua yepi ni matundu ya kweli na yasiyokuwa ya kweli,” anaongezea Paulo.
Kwa mujibu wa Paulo, binadamu anajifunza kupitia kufundishwa na watu wengine nini anapaswa kufanya (operant conditioning ) au kupitia mazingira yaliyomzunguka ( classical conditioning).
Walemavu wa akili wanafundishika?
Kintu Kilanga ambaye ni mwalimu wa walemavu wa akili na wa viungo katika chuo cha Veta ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kundi hilo linafundishika lakini ni lazima mwalimu aweke ubunifu katika kubaini njia sahihi ya kufundisha kwani kila mwanafunzi ana namna yake.
“Kila mwanafunzi anakuja na mtaala wake kwa sababu wametofautiana aina ya ulemavu, unatakiwa kwanza kuelewa nini anahitaji ndipo umfundishe,” anasema Kilanga.
Kilanga anabainisha kuwa lengo la kuanzisha kitengo cha watu wenye mahitaji maalumu katika chuo chao ni kuondoa fikra potofu iliyopo kwenye jamii kuwa mtu mwenye ulemavu hawezi kujifunza.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina walemavu 848,530 wa uoni, viziwi 425,322, walemavu wa viungo 525,019, na 401,931 ni walemavu wa kumbukumbu.
Walemavu wa kushindwa kujihudumia wapo 324,725 huku watu wenye ulemavu mwingine yaani kwa ujumla wake ni 99,798.
Mwalimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika chuo cha Veta Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Kintu Kilanga alipokuwa akiongea na Nukta Habari. PichalEsau Ng’umbi/Nukta
Jamii inaona matokeo chanya
Kwa mujibu wa Kilanga mpaka sasa wamefanikiwa kuwafundisha wanafunzi 80 wenye mahitaji maalumu ambapo kwa sasa ana darasa la wanafunzi 20 wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Hiyo imechangiwa na mwitikio wa jamii wa kuwawezesha watu wenye ulemavu kutekeleza ndoto zao bila vikwazo.
“Wakishatengeneza vitu tulivyowafundisha tunawaruhusu waende navyo nyumbani, ile inawafanya wanajamii kubadili mtizamo wao kuhusu watu wenye ulemavu na baadhi waliokuwa wanaficha watoto wao wanaanza kuwaleta shuleni ili nao wajifunze,” anabainisha Kilanga.
Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa watu wenye ulemavu inabainisha kuwa msimamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu ni kizuizi katika maendeleo yao.
“Msimamo huo unasababisha kutengwa kwa watu wenye ulemavu katika jamii na hivyo kuwafanya washindwe kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla,” inabainisha Sera hiyo.
Sera hiyo ya mwaka 2004 inatamka kuwa upo umuhimu wa kurekebisha mtizamo huu kwa kuwapa nafasi watu wenye ulemavu ili waishi maisha ya kuzalisha na kujitegemea kama wananchi wengine.
Latest



