SGR Dar es Salaam – Dodoma, kuanza rasmi Agosti Mosi 2024
- Kuzinduliwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
- Inatarajiwa kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
- Sekta za biashara, uvuvi, kilimo na ufugaji kunufaika moja kwa moja.
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema uzinduzi rasmi wa safari za treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma utafanyika Agosti Mosi 2024, jambo linaloashiria kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji hali itakayochochea ukuaji wa uchumi.
Uzinduzi huo utafanyika ikiwa imepita siku 49 tangu kuanza kwa safari za SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, zilizoanza kufanyika Juni 14, 2024 ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya ule alioagiza Rais Samia Disemba 31, 2023 ambapo aliutaka uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha safari za SGR zinaanza ifikapo mwezi Julai 2024.
Prof Makame aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Julai 30, 2024 jijini Dar es Salaam, amewaambia kuwa katika uzinduzi huo utakaofanyika jijini Dodoma Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Ni jambo la kujivunia na kuhakiksha kuwa kila mmoja wetu anakuwa mstari wa mbele katika kuitumia na kuitunza reli yetu na kuilinda kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” amesema Mbarawa.
Mbarawa ameongeza kuwa mpaka sasa Tanzania ndio nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na mtandao mkubwa wa reli ya umeme.

Abiria wakiwa ndani ya Treni ya kisasa inayotumia umeme. Picha I Daily News Tanzania
Kwa mujibu wa Prof Mbarawa mpaka sasa Serikali imeshatumia Dola za Marekani Bilioni 3.138 sawa Sh7.84 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya SGR kwa vipande viwili Dar es Salaam- Morogoro na Morogoro – Makutupora mkoani Dodoma kwa vipande viwili vyenye urefu wa kilometa 722.
Prof Mbarawa amewaambia wanahabari kuwa kuanza kwa huduma ya usafiri wa treni ya SGR kunatarajiwa kuongeza ukuaji wa uchumi katika pato la Taifa na pamoja na kuchocheaa maendeleo ya shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala kwa kutoa usafiri wa uhakika na wa haraka.
“Sekta zinazoguswa moja kwa moja na SGR ni biashara, utalii, viwanda, kilimo, uvuvi na ufugaji,” amesema Mbarawa.
Aidha, uwezo wa treni hizo kubeba mizigo wa hadi tani 10,000 kwa mara moja sawa na malori 500 ya mizigo (yenye tani 20) utasaidia kupunguza msongamano wa magari katika bandari ya Dar es Salaam na kupunguza uharibifu wa bara bara.
Soma zaidi: Tanzania yasaka Sh8 trilioni kukamilisha mradi SGR
Treni ya SGR yapewa hadhi
Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa watumiaji wa treni za SGR juu ya kuzuiliwa kuingia na baadhi ya mizigo yao katika treni hizo, Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa amesema utaratibu huo umewekwa ili kuzipa hadhi treni hizo.
“Lazima tuwe na standard(viwango) fulani, treni yetu Watanzania wanachotakiwa kuelewa reli hii ukiipeleka Ulaya au Marekani bado itabaki kuwa katika viwango vya kimataifa…
…wale wenye mizigo na vifurushi wanaweza kupanda treni ile ya kawaida kule tumelegeza kidogo, lakini huku lazima tuwe na hadhi kidogo lazima tuwe na viwango,” amesema Kadogosa.
Kwa mujibu wa muongozo wa TRC abiria anayesafiri katika treni za SGR hatakiwi kuwa na mifuko ya plastiki, silaha, chakula, vinywaji, ndoo, mapipa pamoja na wanyama.
Aidha, mizigo yenye uzito uliopitiliza hairuhusiwi katika treni hizo ambapo abiria wa daraja la biashara anapaswa kuwa na mzigo usiozidi kilo 30, huku daraja la uchumi usizidi kilo 29.
Kwa mujibu wa TRC, miongozo hiyo inalenga kuhakikisha viwango vya usalama na uendeshaji vinazingatiwa.