Mabadiliko ya tabia: Suluhu ya uwindaji haramu wa wanyamapori Tanzania
- Wadau wasema elimu na mabadiliko ya tabia vinaweza kupunguza matukio ya uwindaji haramu.
- Ushirikiano wa wadau na utekelezaji wa sheria ni suluhu nyingine.
Manyara. Watalaam na wadau wa masuala ya wanyamapori wamependekeza kuwekeza katika kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia kwa wananchi wanaokaa karibu na hifadhi za Taifa kama suluhu ya kumaliza biashara na matumizi yasiyo halali ya nyamapori.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009 imeweka bayana kuwa wanyamapori ni sehemu ya nyara za Serikali, hivyo mtu anayetaka kutumia nyamapori ni lazima afuate taratibu za kisheria kuipata ikiwemo kupata kibali maalum.
Licha ya kuwepo kwa taratibu za kisheria za kupata nyamapori, bado wako baadhi ya watu hasa wanaoishi karibu na mbuga za nyama kujipatia kitoweo hicho kwa njia isiyo halali, jambo linaloathiri uhifadhi wa wanyamapori ambao una umuhimu mkubwa katika mazingira na maendeleo ya Taifa.
Kwa kutambua umuhimu wa wanyamapori, shirika lisilokuwa la kiserikali la TRAFFIC Afrika Mashariki limesema suluhu mojawapo ya kumaliza ujangili unaohusisha nyamapori ni kubadilisha tabia za watu kuhusu wanyamapori.
Meneja wa Mabadiliko ya Tabia katika Ofisi ya TRAFFIC Afrika Mashariki, Jane Shuma amesema watu wakielimishwa na kufahamu kwa undani kuhusu tabia za wanyamapori na namna wanavyohusiana na mazingira na maisha ya binadamu itasaidia kupunguza vitendo vya ujangili wa wanyamapori.
“Tabia za watu zinachangia kuendeleza matumizi yasiyo sahihi ya nyamapori, hivyo watu wakielimishwa na kubadilika mtazamo au fikra inaweza kupunguza vitendo hivyo,” amesema Shuma.
Shuma alikuwa akizungumza hivi karibuni mkoani Manyara katika warsha ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na TRAFFIC kwa ufadhili wa shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) chini ya mradi wa CONNECT kwa lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuripoti kwa usahihi habari za biashara na uhifadhi wa wanyamapori nchini.
Shirika hilo linalofanya kazi katika nchi mbalimbali duniani ya ufuatiliaji wa biashara halali na haramu ya viumbepori ikiwemo mimea na mwaka huu wa 2022 litaanza kutekeleza programu maalum ya mabadiliko ya tabia kwa jamii za watu wanaoishi karibu na hifadhi za wanyamapori ili kuwajengea uelewa kuhusu matumizi ya nyamapori.
Tembo ni miongoni mwa wanyamapori ambao wamekuwa hatarini kutoweka kwa sababu wamekuwa wakiwindwa na majangili ili kupata pembe zao na nyama. Hata hivyo, Serikali imedhibiti kwa kiasi kikubwa ujangili wa wanyamapori nchini. Picha| Focus East Africa.
Shuma amesema programu hiyo ikitekelezwa kwa ukamilifu katika maeneo yaliyochaguliwa itasaidia kupunguza vitendo vya ujangili vinavyohusisha ulaji wa nyamapori usiofuata sheria.
Meneja huyo wa mabadiliko ya tabia amesema programu hiyo pia inalenga kusaidia utekelezaji wa mkakati wa kupambana na ujangili, biashara haramu na usafirishaji wa wanyamapori na mazao ya wanyamapori wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Anti-poaching Strategy).
Utekelezaji wa programu hiyo ya mabadiliko ya tabia itaenda sambamba na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wa uhifadhi ikiwemo utekelezaji wa sheria za wanyamapori ili kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mabadiliko ya Tabia (BCAG) iliyo chini ya TRAFFIC, Asha Mtwangi amesema kuwa kazi hiyo ya mabadiliko ya tabia itaanza kwa majaribio katika ushoroba wa Kwakuchinja katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.
Ushoroba wa Kwakuchinja ni mapitio ya wanyamapori kati ya hifadhi za Taifa ya Ziwa Manyara na Tarangire ambao ni muhimu kwa kudumisha mfumo wa ikolojia wa Tarangire-Manyara ambao ni makazi ya wanyamapori.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, walengwa wa programu hiyo ni watendaji wa Serikali, wanawake na wafanyabiashara wa nyamapori huku Serikali itashiriki kuboresha mifumo ya ufuatiliaji pamoja na ugavi.
“Wanawake watashirikishwa kupitia vikundi vya kijamii na taasisi za kidini kuongea nao kuhusu ulaji wa nyamapori iliyovunwa kinyume cha sheria katika kaya zao na majukwaa mengine,” amesema Mtwangi.
Mtwangi amesema ikiwa programu hiyo itafanikiwa itasaidia jamii zinazoishi karibu na hifadhi hasa wanawake kuepuka mkono wa sheria kwa sababu watakuwa na uelewa mpana wa wa bishara ya nyamapori.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Maajabu ya visiwa 11 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Rubondo
Aina nyingine ya ujangili
Hata hivyo, Afisa Programu kutoka TRAFFIC, Allen Mgaza amesema mbali na ujangili wa nyamapori, ipo aina nyingine ya ujangili inayofanyika nchini ikihusisha sehemu/viungo vya wanyamapori vikiwemo mikia, kucha na ngozi za wanyama hao.
“Biashara hiyo mara nyingi hufanyika kwa mtandao wa watu wanaofahamiana na kuaminiana,” amesema Mgaza.
Mtaalam huyo wa wanyamapori amesema viungo hivyo hutumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo matambiko, utamaduni, mila na kutengeneza dawa za kienyeji.
Mgaza amesema utafiti unahitajika zaidi kubaini undani wa aina hiyo ya ujangili na jinsi unavyofanyika ili kubuni njia sahihi za kudhibiti.
Washiriki wa warsha ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na TRAFFIC mkoani Manyara hivi karibuni kwa ufadhili wa shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) chini ya mradi wa CONNECT kwa lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuripoti kwa usahihi habari za biashara na uhifadhi wa wanyamapori nchini. Picha| Daniel Samson.
Mambo yanayochangia ujangili wa nyamapori
Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati mkaoni Manyara, Christopher Laizer amesema wakati mwingine uwindaji haramu wa wanyamapori husababishwa na kutopatikana kwa wakati na kupanda kwa bei ya nyamapori katika mabucha yanayotambulika na Serikali.
“Kwenye mabucha utakuta nyama inauzwa Sh8,000 lakini hiyo ya mtaani (isiyo halali) inauzwa Sh2,000. Sasa watu wanakimbilia bei ndogo na hivyo kuendelea kuwinda kwa njia haramu,” amesema Laizer.
Mtaalam huyo wanyamapori amesema sababu nyingine ni mazoea ya baadhi ya watu kula nyamapori na wasipoipata kwa wakati na njia halali hujikuta wakiingia katika mtego wa kuwinda kwa njia haramu.
Mazoea hayo yanachagizwa na mila na desturi za watu hasa wanaoishi karibu na hifadhi kupenda nyama hiyo.
Mhandhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi wa Wanyamapori ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Alfan Rija amesema umaskini na ukosefu wa ajira kwa vijana huwasukuma kuingia katika biashara haramu ya wanyamapori.
“Kuna umuhimu wa kuanzisha miradi ya kiuchumi kuwasaidia watu wanaoishi katika maeneo ya hifadhi ili kujipatia kipato na kuondokana na umaskini,” amesema Dk Rija na kusema njia hiyo itapunguza tatizo la ujangili kwa ajili ya nyamapori.
Naye, Afisa Mhifadhi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wibright Munuo amesema wanaendelea kutoa elimu na kutekeleza sheria zinazosimamia wanyamapori ili kuhakikisha viumbe hao wanakuwa salama wakati wote.
Latest