Mambo yatakayosaidia uhifadhi endelevu wa wanyamapori Tanzania

December 3, 2021 8:20 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu uhifadhi.
  • Waandishi wa habari kutumia kalamu zao kutoa taarifa sahihi.
  • Ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya uhifadhi.

Dar es Salaam. Ili kuwa na uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini Tanzania, jamii imetakiwa kupewa elimu ya kutosha na kushirikishwa kikamilifu katika mikakati ya kukabiliana na vitendo vinavyotishia uhai wa wanyama hao.

Wanyamapori ni sehemu ya mazingira hivyo wakihifadhiw na kutunza vizuri katika maeneo yao itasaidia kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, wadau wa mazingira wameeleza kuwa elimu hiyo itafika kwa urahisi ikiwa waandishi wa habari watajengewa uwezo wa kuandika kwa usahihi habari zinazohusu uhifadhi wa wanyamapori. 

Mapendekezo hayo yametolewa na watalaam wa mazingira na wanyamapori katika warsha ya siku tatu kwa waandishi wa habari iliyofanyika Novemba 23 hadi 25, 2021 jijini Dar es Salaam.

Warsha hiyo ililenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari  kuripoti kwa usahihi habari zinazohusu uhifadhi, uwindaji haramu wa wanyamapori na usafirishaji na zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk Hellen Otaru ambao ndiyo waandaaji wa warsha hiyo amesema waandishi wa habari ni wadau muhimu kuongeza uelewa wa uhifadhi wanyamapori Tanzania.

“Kalamu zenu zina umuhimu sana katika suala hili,” amesema Dk Otaru wakati wa kufungua warsha hiyo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa “Tuhifadhi Maliasili” unaosimamiwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na shirika la kitamataifa la utafiti la RTI. 

Dk Ottaru amesema waandishi wa habari wakiripoti kwa usahihi itasaidia kupunguza migogoro ya binadamu na wanyama kwa sababu itapatikana suluhu ya namna ya kutatua migogoro hiyo katika maeneo yao.

Katika warsha hiyo, mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo njia za kisasa za uhifadhi wanyamapori, mabadliko ya tabianchi, tabia na mitazamo ya watu kuhusu wanyamapori na ushirikishwaji wa wananchi katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori.

Pia wanahabari hao walifundishwa mbinu na zana za kidijitali za kuripoti habari za uhifadhi kutoka kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Afrika.

Baadhi ya washiriki wa warsha ya siku tatu kwa waandishi wa habari iliyofanyika Novemba 23 hadi 25, 2021 jijini Dar es Salaam. Picha| Nyamiti Kayora.

Meneja wa ushirikishwaji wa sekta binafsi wa RTI na Mkandarasi wa USAID anayetekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili, Dk Elikana Kalumanga amesema ni muhimu kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu ya uhifadhi wa wanyamapori ambayo itasaidia kutoa suluhu ya kila changamoto inayoibuka wakati wa uhifadhi.

Dk Kalumanga ametolea mfano wa mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuchangia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hivyo kuna umuhimu wa kutafuta suluhu la suala hilo ili pande zote mbili ziweze kufaidika na maliasili. 

Aidha, amewashauri watu kuwa na uelewa mpana wa wanyamapori na kuona kuwa uwepo wao una umuhimu katika mazingira na maisha yao. 

Baada ya warsha hiyo, waandishi walioshiriki watapata fursa ya kutembelea baadhi ya ushoroba zilizopo nchini ili kujifunza namna wanyamapori wanavyohusiana na binadamu katika mapitio yao.

Ushoroba hizo ni pamoja na Kwakuchinja, Tarangire-Simanjiro, Kigosi Moyowasi-Uvinza, Nyerere Selous-Udzungwa na Amani Nilo. 

Licha ya mafunzo hayo, mradi wa Tuhifadhi Maliasili utawakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi na Serikali katika mijadala na mashauriano ya kutafuta namna bora za uhifadhi wa wanyamapori Tanzania.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW