Lissu: Serikali haikutishwa, hivyo hakuna kosa la uhaini
- Asema upande wa mashtaka ulipaswa kutaja wazi ni taasisi au kiongozi gani wa Serikali aliyedaiwa kutishiwa.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa aliitishia Serikali, hivyo kwa maoni yake hana kesi ya kujibu.
Lissu anayeshtakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 ametoa hoja hiyo leo, Septemba 25, 2026, akiendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Katika hoja zake za mwisho, Lissu amesema upande wa mashtaka ulipaswa kutaja wazi ni taasisi au kiongozi gani wa Serikali aliyedaiwa kutishiwa na kuthibitisha kwa ushahidi kuwa matamshi yake yalilenga kuitisha Serikali.
Kiongozi huyo wa upinzani amedai kuwa upande wa mashtaka haukuonyesha katika ‘information’ namna Serikali ilivyodaiwa kutishiwa, wala haukuleta ushahidi unaoonyesha jinsi Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilivyotishwa.
“Upande wa mashtaka hawakuonyesha kwenye hati yao ya mashtaka na hiyo peke yake inafanya hati ya mashtaka kuwa batili. Vilevile hawakuleta ushahidi wowote wa kuonyesha jinsi Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilivyotishiwa.”

Kwa mujibu wa Lissu, suala hilo ni muhimu kwa sababu upande wa mashtaka ndio uliokuwa na wajibu wa kuthibitisha vipengele vya kosa analokabiliwa nalo, si upande wa utetezi kuthibitisha kwamba Serikali haikutishwa.
“Kama hakuna ushahidi, maana yake ni kwamba haikutishika. Na kama haikutishika, sina kosa.”
“Vigogo wa Serikali, walikwamisha ushahidi”
Katika hoja nyingine, Lissu amezungumzia kutokuwepo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ambao kwa mtazamo wake, wangeweza kutoa ushahidi iwapo Serikali ilitishwa au la.
Viongozi hao ni Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais Philip Mpango na aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambao walitajwa na Lissu kama miongoni mwa mashahidi 11 wa utetezi katika kesi hiyo kabla ya mahakama kutupilia mbali ombi hilo Septemba 10 mwaka huu.
Hata hivyo, majaji hao waliagiza kuitwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai ambao pia baadae walikataa kumtetea Lissu
Kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi huo, Lissu ameiomba Mahakama izingatie kile alichokiita ‘negative inference’ yaani kutoa hitimisho kutokana na kushindwa kwa upande wa mashtaka kuleta ushahidi au mashahidi waliokuwa muhimu kwa hoja hiyo.
Lissu anatarajiwa kuhitimisha majumuisho ya hoja za utetezi Septemba 28, mwaka huu, kabla ya upande wa mashtaka kuwasilisha majumuisho yao, hatua itakayofungua njia kwa Mahakama kutoa uamuzi iwapo ana hatia katika kesi ya uhaini inayomkabili, ambayo adhabu yake kwa mujibu wa sheria ni kifo ama ataachiwa huru.