Mahakama Kuu Tanzania yaanza kusikiliza ushahidi kesi ya Lissu
- Lissu alipinga sehemu ya ushahidi huo akidai kuwa maneno yaliyodaiwa na shahidi si sehemu ya shtaka la uhaini linalomkabili.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imeanza kusikiliza ushahidi wa kesi yake ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ikiwa ni takriban miezi sita tangu afunguliwe mashtaka hayo.
Leo mahakama hiyo imeanza kusikiliza ushahidi kutoka upande wa Jamhuri ambao utatakiwa kuthibitisha tuhuma dhidi kiongozi huyo wa upinzani nchini. Waendesha mashtaka walieleza kuwa watawasilisha mashahidi takribani 30, huku upande wa utetezi wa Lissu ukitarajia kuita mashahidi 15, wakiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na viongozi wengine wa juu wa serikali.
Kusikilizwa kwa ushahidi huo kunafuatia hatua ya awali ambapo Lissu alisomewa maelezo ya awali (PH) mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.
Septemba 22 mwaka huu baada ya kusomewa maelezo ya awali Lissu alikiri wasifu wake ikiwemo jina, makazi na kazi, lakini alikana kutenda kosa la uhaini.
Kesi hiyo ya uhaini inamkabili Lissu kutokana na tuhuma kwamba Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam akiwa raia wa Tanzania, alitoa matamshi yenye nia ya uchochezi yaliyodaiwa kuwahamasisha wananchi kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Leo, Jumatatu Oktoba 6, Lissu amefikishwa tena mahakamani ambapo kesi yake ilisikilizwa kwa mara ya kwanza, kabla ya kuahirishwa hadi kesho, Oktoba 7, 2025. Kwa mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani, kesi hiyo itasikilizwa mfululizo hadi Oktoba 24, 2025.
Katika hatua ya awali ya usikilizwaji wa ushahidi, Lissu ameibua mapingamizi mara mbili dhidi ya shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, Kamishna Msaidizi wa Polisi George Bagemu, ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DZCO) Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Pingamizi hilo lilitolewa wakati shahidi huyo alipotoa ushahidi wake kuhusu kipande cha video kinachomuonesha Lissu akizungumza maneno yaliyomo kwenye hati ya mashtaka.
Lissu alipinga sehemu ya ushahidi huo akidai baadhi ya maneno yaliyodaiwa na shahidi si sehemu ya shtaka la uhaini linalomkabili.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilitupilia mbali hoja za Lissu na kukubaliana na upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga, aliyedai kuwa ni jukumu la mahakama kuamua iwapo ushahidi huo una uhusiano na shtaka husika.
Ushahidi wa mashahidi wengine unatarajiwa kuendelea kesho katika Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam.
Latest



