Kutoka vyuma chakavu hadi mashine ya kupukuchua mahindi
- Adam Kinyekile (47) ndiye aliyebuni mashine hiyo mwaka 2019 katika karakana ndogo eneo la Mpemba mkoani Songwe.
- Saizi ndogo ya mashine hiyo inauzwa kwa Sh1.5 milioni na Sh12 milioni kwa saizi kubwa.
Songwe. Wakati mamia ya vyuma chakavu vikiishia katika mlundikano wa taka au vijiwe vya kupima vyuma mtaani, kwa Adam Kinyekile (47) ni dhahabu iliyobadili maisha yake.
Kila anapoona mabaki ya vyuma hivyo, Kinyekile huona mwanzo mpya wa bidhaa inayoweza kuwasaidia wakulima na kumuingizia kipato.
Baada ya kutamba na bunifu mbalimbali zilizotengenezwa na vyuma chakavu ikiwemo gereji inayotembea mwaka 2016, Kinyekile amebuni tena mashine ya kupukuchulia mahindi ambayo ni mkombozi kwa wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani za Malawi na Zambia.
Mbunifu huyo anasema wazo la kutengeneza mashine hiyo lilikuja baada ya kubaini changamoto ya kupukuchua mahindi kwa mrefu wanayokumbana nayo wakulima
‘’Nilifanya utafiti mdogo na kugundua kuwa watu wengi wanapoteza muda shambani, huku wakitumia nguvu nyingi lakini matokeo madogo, ndipo nilipamua kutumia vyuma chakavu kutengeneza mashine hii ambayo imekuwa mkombozi kwa mkulima,’’ amesema Kinyekile.

Kwa undani mashine ya kupukuchua mahindi
Ubunifu wa mashine hiyo ulianza rasmi mwaka 2019 katika karakana ndogo eneo la Mpemba mkoani Songwe na ndani ya mwaka huo huo ilianza kuingia shambani na kuwasaidia wakulima.
Mashine aliyobuni Kinyekile ina uzito wa takriban kilo 700 hadi 900 ikiwa imeunganishwa na guta ya chuma ya miguuu mitatu inayoiwezesha kutembea kwa urahisi kuwafikia wakulima hususani wakati wa mavuno.
Tofauti na ilivyo kwa wakulima wengi ambao hutumia siku, wiki au miezi kupukuchua mahindi kwa mkono au kuyapinga kwa fimbo, mashine hiyo ina uwezo wa kupukuchua takribani magunia 1,000 kwa saa moja.
Hii ina maana mkulima anaweza kutumia saa kadhaa kumaliza zoezi la kupukuchua mahindi tofauti njia nyingine ambazo huchukua muda mrefu.
Mashine hii inaweza kuwa mkombozi kwa wakulima wadogo na wakubwa ambao wanalima eneo pana, pia inatajwa kuwa ni nyenzo muhimu kwa wakulima na wawekezaji wanaofanya kilimo biashara.
Mbali na kupukuchua mahindi, mashine hiyo ina uwezo wa kuchakata mabaki ya mazao kwa ajili chakula cha mifugo pamoja na malighafi kwa ajili ya kutengeneza mbolea pamoja na kusaidia pia katika shughuli ya uvutaji maji.

Ukiwa na mashine hiyo kwa mujibu wa Kinyekile, utakuwa na uwezo wa kuvuta hadi mita 50 kutoka kwenye chanzo na kuyapeleka katika eneo analohitaji mkulima kwa ajili ya umwagiliaji.
Ili uweze kuipata mashine hiyo utalazimika kutoboa mfuko wako hadi Sh1.5 milioni kwa saizi ndogo na Sh12 milioni kwa saizi kubwa.
“Gharama ya kutengeneza mashine moja kubwa yenye umbo la guta ni Sh milioni 12, wakati mashine nyingine ndogo zinazoweza kupakiwa kwenye pikipiki hugharimu Sh milioni 1.5. Mashine hizo ninazikodisha kwa wahitaji au kuzitengeneza kwa mtu anayehitaji,” amesema Kinyekile.
Changamoto bado zipo
Licha ya umuhimu wa mashine hiyo, bado uzalishaji wake ni mdogo hali inayowafanya mamia ya wahitaji kuikosa.
“Mahitaji ni makubwa, wakulima kila siku wanakuja na kunitafuta wakihitaji mashine, lakini changamoto ni kwamba siwezi kutengeneza mashine nyingi kwa wakati mmoja kutokana na shughuli nyingine ninazofanya,” amesema.
Kwa mujibu wa Kinyekile, changamoto kubwa anayokumbana nayo inafanana na wabunifu wengine ambayo ni utitiri wa mamlaka za udhibiti na usajili ambazo zimekuwa kikwazo kutimiza ndoto za wabunifu.
Ametolea mfano, mashine yake ina muundo wa chombo cha moto na inasafiri kwa kutumia barabara hivyo inahitaji usajili kutoka mamlaka nyingine ikiwemo Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA).
‘’Costech wao wamewezesha ubunifu, lakini inapofika suala la kuendeleza, kujaribu, kutumia na kuuza teknolojia tunakutana na taasisi nyingine ambazo zimekuwa kikwazo au mchakato wake unachukua muda mrefu hadi kufika mwisho wa kazi zetu,’’ anasema

Inaokoa gharama
Kwa mujibu wa Kinyekile, mashine hiyo hutumia takribani lita moja ya dizeli kupukuchua magunia 1,000 ya mahindi kwa saa.
Hivyo ili uweze kupukuchua kiwango hicho cha mahindi utalazimika kulipa Sh4,054 ya dizeli kwa mujibu wa bei mpya za mwezi Septemba, 2026 zilizotolewa na Mamlaka ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zinazotumika mkoani Songwe.
Hii ina maana ukitumia mashine kwa siku nzima utatoboa mfuko hadi Sh48,648 kwa siku moja au Sh340,536 ikiwa utaitumia kwa wiki nzima.
Aliko Kibona, mkulima na mkazi wa Ihanda, mkoani humo amesema mashine hiyo imemrahisishia kazi ya kupukuchua mahindi na kumpunguzia gharama.
“Mashine hii imetusaidia sana sisi wakulima kwa sababu kazi ambayo zamani ilikuwa inachukua muda na nguvu nyingi, sasa tunamaliza kwa muda mfupi zaidi,” amesema Kibona.
Kwa upande wake Juliana Mwampashi, anasema mashine hiyo imempunguzia mzigo wa kufanya kazi za shambani na kumuwezesha kufanya shughuli nyingine za malezi na uchumi.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kuendeleza na Kuhawilisha Teknolojia cha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Erasto Mlyuka, amesema taasisi hiyo inajivunia kumuunga mkono mbunifu huyo kwa kumwezesha kifedha na kitaalamu ili kuendeleza bunifu zake.
Aidha, amesema taasisi hiyo ilimuunganisha na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Tawi la Myunga, Wilaya ya Momba, ambayo imeendelea kufuatilia maendeleo ya ubunifu wake na kumpa ushauri wa kitaalamu.