Katambi alivyouzima mgomo wa mabasi Stendi ya Magufuli
- Ni baada ya madereva wa mabasi kugoma kwa takribani saa 11
- Aagiza kusitisha kwa mfumo wa pointi, madera kurudishiwa leseni.
Dar es Salaam/ Arusha. Hatimaye mgomo wa madereva wa mabasi katika Stendi ya Magufuli jijini Dar es Salaam umesitishwa baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kuzungumza na madereva hao na kutoa maagizo ya kushughulikia malalamiko yao.
Mgomo huo ulioanza leo Jumanne, Septemba 29, 2026, saa 12:00 asubuhi ulizifanya shughuli za usafirishaji wa abiria kukwama katika stendi hiyo, hali iliyosababisha abiria waliokuwa wakisubiri usafiri kukaa kwa muda bila huduma.
Takriban saa 11 baada ya kuanza kwa mgomo huo Waziri Katambi aliwasili katika stendi hiyo kusikiliza malalamiko ya madereva hao na kutoa maagizo ya Serikali yaliowapoza machungu.
“Mimi naahidi kuwa balozi wenu…tutakuwa watu wa hovyo kama hatutasikiliza changamoto hizi, ujenzi wa uchumi unahusisha pia madereva kwa kiwango kikubwa kwahiyo hili sio jambo la kupuuza na tunalipa uzito mkubwa,” amesema Katambi.
Sababu ya mgomo
Akizungumza mbele ya Waziri Katambi Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania Majula Kafumu, amezitaja baadhi ya sababu za mgomo huo kuwa ni pamoja na kukatwa kwa pointi, kufungiwa kiholela leseni, miundombinu mibovu ya barabara, pamoja na mfumo wa VTS kutosimamiwa vizuri..
Awali, Adam Patrick, mmoja wa madereva walioshiriki katika mgomo huo aliiambia Nukta Habari kuwa kukatwa point kunawakandamiza madereva kiasi cha kuwafanya kushindwa kufanya shughuli zao.
“Kama yupo dereva wa Tanzania hii ambaye atakubali suala la kukatwa point, kwa namna nnavyopata tabu katika utoaji wa huduma hii aje achukue gari” amesema Patrick.
Kukatwa point ni nini
Kukatwa pointi ni mfumo wa kufuatilia makosa ya madereva kwa kupunguza pointi kwenye leseni kulingana na aina na uzito wa kosa la barabarani.
Msingi wake umewekwa katika Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, kwa lengo la kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kupunguza ajali, vifo na madhara yanayotokana na ajali za barabarani.
Utaratibu huo uliwekwa mahsusi kupitia Kanuni za Usalama na Matumizi ya Barabara (Drivers Licence Point System), 2014, zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 109 la mwaka 2014 na baadaye kufanyiwa marekebisho kutokana na maoni ya wadau wa sekta ya usafirishaji.
Chini ya mfumo uliorekebishwa, dereva hupewa pointi 15 ambazo hupungua anapobainika kufanya makosa yaliyoainishwa katika kanuni hizo.
Kutokana na mfumo huo kupigwa mawe na madereva wengi Katambi leo amerejea uamuzi wake wa Septemba 19, 2026 akitaka utaratibu huo kusitishwa hadi utakapofanyiwa tathmini.
“Vyombo vya dola, vya usalama visimkate dereva yoyote pointi na kama kuna mtu aliyekatwa pointi nileteeni majina ofisini ashughulikiwe,” amesisitiza Katambi.
Aidha, Katambi ametoa maagizo mengine ikiwemo kuboresha utaratibu wa kubaini makosa, kukomesha uonevu kwa madereva, kuweka viashiria sahihi kwenye barabara zinazojengwa na kurejesha leseni zilizochukuliwa na askari wa usalama barabarani.
Kiongozi huyo pia ameomba siku 14 kwa ajili ya kushughulikia changamoto nyingine za kisekta.
Nyongeza na Lucy Samson