Watalii wa ndani waongezeka hifadhi ya Taifa ya Saanane
- Licha ya Corona, idadi ya watalii yaongezeka kwa asilimia 30.
- Matangazo na hamasa yasaidia kuongeza idadi hiyo.
Mwanza. Licha ya kuwepo kwa janga la Corona (Uviko-19), Hifadhi ya Taifa ya Saanane imeendelea kujiimarisha katika kujitangaza na kufanikiwa kuongeza idadi ya watalalii wa ndani kwa asilimia 30.
Janga la Uviko-19 lilisababisha shughuli za usafiri wa kimataifa kupungua na hivyo kuathiri idadi ya watalii wa kimataifa waliokuwa wanaingia Tanzania.
Kutokana na athari hizo, uongozi wa hifadhi hiyo ya kisiwa cha Saanane ulielekeza nguvu zake katika kuvutia watalii wa ndani kwa kuongeza matangazo na hamasa kwa wananchi.
“Idadi wa watalii imeongezeka kutokana na kufanya uhamasishaji ambapo makundi na taasisi mbalimbali kutembelea eneo hilo,” amesema Mkuu wa hifadhi hiyo, Eva Mallya.
Kwa mujibu wa Mallya, idadi ya watalii katika hifadhi hiyo wameongezeka kwa asilimia 30 mwaka mmoja uliopita.
Mwaka 2019/20 watalii wa ndani waliotembelea hifadhi hiyo walikuwa 13,264 na imeongezeka hadi watalii 19,132 mwaka 2020/21.
Amesema kwa sasa watalii wa ndani wameongezeka baada ya kutambua umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyomo nchini.
Hifadhi hiyo ya saanane inaendelea kutoa fursa mbalimbali za kitalii hususani katika kipindi hiki cha Uviko 19 ambapo watalii wanafanya matembezi, michezo na kupumzika katika kambi.
Pia ukiwa katika hifadhi hiyo iliyopo Ziwa Victoria unaweza kuwaona wanyama mbalimbali ikiwemo simba, ndege aina ya tausi , swala, papa na pundamilia.
Afisa uhifadhi wa wanyamapori katika kisiwa hicho, Hilda Mikongoti amesema mbali na watalii kuona wanyama pia itawasaidia watalii kujifunza masuala ya mazingira na viumbe hai.
Jinsi ya kuongeza idadi ya watalii wa ndani
Ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani, wadau wa masuala ya utalii wameishauri Serikali kuangalia gharama za kuingia maeneo ya hifadhi zitakazoendana na hali halisi ya maisha ya Watanzania kwa sasa.
Mdau wa masuala ya utalii Elisha mkoani Mara, Mwiteki amesema katika kipindi hiki cha Uviko-19, Serikali inaweza kushusha zaidi gharama ili kuvutia idadi kubwa ya watu kuliko kuwasubiri watalii wa nje.
“Tanzania tumejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, na umuhimu wa kuwa na vivutio nchini ni pamoja na wananchi kuvitembelea ili kuongeza pato la Taifa kuliko kutegemea wageni kutoka nje peke yake,” amesema Mwiteki.
Pia elimu itolewe kwa wananchi hasa wanafunzi kujua umuhimu kuthamini maliasili zao na kuzitembelea ili kujifunza mambo mapya ambayo hayapatikani katika maeneo yao.
“Vilabu mbalimbali viundwe kuanzia shuleni na watoto wafundishwe umuhimu wa kulinda na kutunza vya kwao, elimu hii ikitolewa itasaidia kuongeza idadi ya watalii wa ndani,” amesema.
Makala haya ni sehemu ya mfululizo ya ripoti maalum zinazoangazia namna ya kukabiliana na Uviko-19 nchini zinazofadhiliwa na Shirika la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).
Latest
