Kila sekunde 100, mtoto mmoja aliambukizwa VVU mwaka 2019 – Unicef
- Hali hiyo imesababisha idadi ya watoto wanaoishi na VVU kufikia milioni 2.8.
- Takribani watoto 110, 000 walifariki kwa Ukimwi katika mwaka huo wa 2019.
- Serikali zatakiwa kuchukua hatua za haraka kuwanusuru watoto.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) imeeleza kuwa takribani kila dakika moja na sekunde 40, mtoto au kijana chini ya umri wa miaka 20 alikuwa anaambukizwa virusi vya Ukimwi mwaka 2019 duniani, jambo linalohitaji elimu kuokoa nguvu kazi inayopotea kwenye ugonjwa huo.
Ripoti hiyo imekuja siku chache kabla ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo huadhimishwa Desemba 1 kila mwaka ili kutoa fursa ya kutafakari hatua zilizofikiwa katika kutokomeza ugonjwa huo.
Ripoti hiyo ya ufikiriaji mpya wa ushughulikiaji wa VVU (Virusi vya Ukimwi) iliyotolewa Novemba 25, 2020 inaeleza kuwa watoto wanaachwa nyuma katika vita dhidi ya VVU ulimwenguni.
Hali hiyo ya kuachwa nyuma, imesababisha ongezeko la maambukizi na hadi kufikia 2019, idadi ya watoto wanaoishi na VVU ilifikia milioni 2.8.
“Takribani watoto 110, 000 walifariki kwa Ukimwi katika mwaka huo wa 2019,” imesema ripoti ya UNICEF inayoangazia mwenendo wa HIV ulimwenguni.
Licha ya jitihada mbalimbali katika mapambano ya muda mrefu dhidi ya VVU na Ukimwi, bado bara la Afrika linaongoza kwa watu wake kuathiriwa na ugonjwa huo usio na dawa wala kinga.
“Hata wakati ulimwengu ukipambana katikati ya janga linaloendelea ulimwenguni (Covid-19), mamia ya maelfu ya watoto wanaendelea kupata mateso ya janga la VVU,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore wakati wa uzinduzi wa ripoti ya VVU na kuongeza kuwa,
“Bado hakuna chanjo ya VVU. Watoto bado wanaambukizwa kwa viwango vya kutisha, na bado wanakufa kutokana na Ukimwi. Hii ilikuwa hata kabla ya Covid-19 kukatiza huduma muhimu za matibabu ya VVU na kinga kuweka maisha mengi zaidi katika hatari.”
Ripoti hiyo inazitaka Serikali zote kulinda, kudumisha na kuharakisha maendeleo katika kupambana na VVU miongoni mwa watoto kwa kudumisha huduma muhimu za afya na kuimarisha mifumo ya afya.
Zinazohusiana:
- Tiba shufaa inavyookoa gharama za matibabu kwa wagonjwa nchini
- Ukimwi kupungua kwa asilimia 75 ifikapo 2020
Tanzania kutunisha mfuko wa Ukimwi
Wakati Tanzania ikiungana na dunia kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani, wadau wa maendeleo na wananchi wametakiwa kuchangia pesa ili kutunisha Mfuko wa udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF).
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghirwa amesema mfuko huu ni muhimu katika kukabiliana na upungufu wa rasilimali za udhibiti Ukimwi pamoja na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
“Nawaomba wananchi wenzangu tuchangie mfuko huu na uchangiaji huu uwe endelevu tushikamane tuwajibike kwa pamoja,” amesema Mghirwa jana mkoani humo ambako maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa.
Amefafanua kuwa takwimu zinaonyesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 40 ya maambukizi mapya, huku akiwataka kuchukua tahadhari na kupata elimu sahihi na njia za kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kongamano kubwa la kisayansi linalowakutanisha wataalamu wa afya kujadili mafanikio, changamoto na namna ya kukabiliana na kudhibiti maambukizi mapya ya VVU nchini Tanzania.
Latest