Ukimwi kupungua kwa asilimia 75 ifikapo 2020

December 2, 2018 6:29 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2018/19 – 2022/23, Jijini Dodoma jana. Picha| ITV


  • Mkakati huo umezinduliwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma.
  • Matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia 5 ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia 2 ifikapo mwaka 2030.
  • Matayarisho yake yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2013/14 – 2017/18.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2018/19 – 2022/23 ambao unatarajia kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2023.

Matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia 5 ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia 2 ifikapo mwaka 2030.

Majaliwa amezindua mkakati jana (Desemba 1, 2018) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma na kusema kuwa matayarisho yake yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2013/14 – 2017/18.

Mbali na matokeo hayo pia mkakati huo utawezesha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na Ukimwi  kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 70 ifikapo mwaka  2023 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo 2023 na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030. 

Hata hivyo, Majaliwa amesema mkakati huo umewianisha na kupanga programu mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa zikiwemo afua zinazotekelezwa kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa Ukimwi (PEPFAR).

“Pia Mfuko wa Dunia wa kudhibiti Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Globa Fund) na jitihada nyingine za makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi mbalimbali na ili kupata matokeo mazuri tunapaswa kuimarisha mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau wote sambamba na kufuata na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: Tiba shufaa inavyookoa gharama za matibabu kwa wagonjwa nchini.


Majaliwa amesema maadhimisho hayo husaidia kubaini changamoto, mafanikio na kutengeneza mikakati ya kupambana na maambukizi ya VVU na Ukimwi

 “Siku hii hutoa fursa kote Duniani kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano ya Ukimwi kwenye jamii zetu,” amesema Majaliwa.

Juni mwaka huu Serikali ilizindua kampeni ya “FURAHA YANGU” akiwa na lengo la kuendeleza mapambano dhi ya ugonjwa huo katika jamii.  

Amesema takwimu zinaonesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “FURAHA YANGU” katika mikoa yote nchini wananchi 262,114 walijitokeza kupima VVU, wakiwemo wanawake 136,389 na wanaume 125,725.

Natoa wito kwa Mikoa na Wilaya zote kuwa kampeni hii iwe endelevu. Viongozi katika ngazi mbalimbali tuungane kwenye uhamasishaji wa jambo hili kwani vita dhidi ya VVU na Ukimwi inahitaji dhamira ya dhati na tafakuri ya kina katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya,” amesisitiza Majaliwa.

Serikali itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za upimaji wa VVU, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa Ukimwi.

Enable Notifications OK No thanks