UNICEF: Matibabu ya VVU kwa watoto, vijana yamepungua
- Watoto na Vijana 110,000 walifariki dunia mwaka 2021 kutokana na sababu zinazohusiana na Ukimwi
- Watoto na vijana wanajumuisha asilimia 17 ya vifo vyote vilivyohusiana na Ukimwi.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema matibabu ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa vijana na watoto yamepungua kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita huku idadi ya maambukizi mapya ikiongezeka.
Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEFya masuala ya Ukimwi iliyotolewa Novemba 28, 2022 jijini New York, Marekani inasema upungufu wa matibabu kwa makundi hayo duniani umesababisha vijana na watoto kuanzia umri wa 0 mpaka 19 kupoteza maisha.
“Takribani vijana na watoto 110,000 wa umri wa miaka 0-19 wamekufa kutokana na sababu zinazohusiana na Ukimwi kwa mwaka 2021,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inafafanua zaidi kuwa maambukizi mapya ya VVU kwa vijana 310,000 yameripotiwa kwa mwaka 2021 na kufanya idadi ya vijana wenye VVU duniani kufikia milioni 2.7.
Licha ya maambukizi hayo kuchangia asilimia saba tu ya watu wote wanaoishi na VVU duniani, watoto na vijana wanajumuisha asilimia 17 ya vifo vyote vilivyohusiana na Ukimwi na asilimia 21 ya maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka 2021.
Anurita Bains, Mwakilishi wa UNICEF kuhusu masuala ya VVU na Ukimwi anasema hali ya kupungua kwa kwa huduma za ugonjwa huo kwa watoto na vijana ndani ya miaka mitatu iliyopita siyo jambo la kawaida na linaweza kuweka makundi hayo kwenye hatari ya magonjwa na vifo.
“Watoto wanaathirika vibaya kwa sababu kwa pamoja tunashindwa kuwapata na kuwapima na kuwapatia matibabu ya kuokoa maisha. Kila siku inayopita bila maendeleo, zaidi ya watoto na vijana 300 hupoteza vita vyao dhidi ya Ukimwi.” ameongeza Bains.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa huduma zinazotolewa kwa watu wazima wanaoishi na VVU ni asilimia 76 ambayo ni asilimia 20 zaidi ya huduma wanayopatiwa watoto.
Soma zaidi
Mapambano dhidi ya VVU,bado kuna matumaini
Hata hivyo, ripoti hiyo ya UNICEF inaonyesha kuwa mwelekeo wa muda mrefu wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo bado ni mzuri.
Maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto wadogo wa umri wa miaka 0-14 yalipungua kwa asilimia 52 kati ya mwaka 2010 hadi 2021, na maambukizi mapya kati ya vijana wa umri wa miaka 15-19 pia yalipungua kwa asilimia 40.
“Vile vile, matibabu ya kurefusha maisha miongoni mwa wanawake wajawazito wanaoishi na VVU iliongezeka kutoka asilimia 46 hadi asilimia 81 katika muongo mmoja uliopita,” imesema ripoti hiyo.
Riipoti hiyo inasema kunatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na janga la Uviko-19 na majanga mengine ya kimataifa, ambayo yameongeza unyanyapaa na umaskini, lakini pia ni taswira ya utashi wa kisiasa unaofifia na hatua za kukabiliana na ukimwi kwa watoto.
“Ulimwenguni kote, asilimia ndogo ya watoto wanaoishi na VVU walipata matibabu ambayo ni asilimia 52 ambayo imeongezeka kidogo sana katika miaka michache iliyopita,” imesema ripoti hiyo.
Latest