Kicheko, kilio bei ya mazao ya chakula ikisalia juu
- Mahindi, mchele, maharage bado bei haishikiki Tanzania
- Bei yasalia juu licha ya kuanza kwa msimu mpya wa mavuno baadhi ya maeneo
Dar es Salaam. Huenda wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya chakula hususani mahindi, mchele pamoja na maharage wakaendelea kutabasamu kutokana na bei ya mazao hayo kuwa juu licha ya msimu mpya wa mavuno kuwa umeshaanza katika baadhi ya maeneo nchini.
Kupanda kwa bei ya bidhaa hizo kunawaumiza walaji kwa sababu wanalazimika kutoboa zaidi mifuko yao zaidi ili kupata mazao hayo ya chakula, wakati wakulima na wafanyabiashara wananeemeka na bei hiyo.
Taarifa mpya ya bei za mazao iliyotolewa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji leo Mei 6, 2023 inaonesha kuwa wakazi wa Dar es Salaam ndio watanunua mahindi kwa bei ya juu zaidi yaani Sh 135,000 hadi 150,000 kwa kilo 100 huku wakazi waSumbawanga Mkoani Rukwa wakinunua kwa Sh 60,000 hadi 65,000.
Hiyo ni kumaanisha kuwa wakazi wa Dar s Salaam wananunua mara mbili ya bei wanayonunulia wakazi wa Sumbawanga.
Bei ya mchele nayo haijapoa hususan katika Mkoa wa Lindi ambako wananunua kilo 100 kwa kati ya Sh200,000 hadi Sh 380,000 ambayo ndio ya juu zaidi wakati wakazi wa Sumbawanga na Mara wakinunua kilo hizo hizo kwa Sh 200,000 hadi 220,000.
Kwa upande wa maharagwe kilogram 100, jijini Dar es Salaam utauziwa kati ya Sh350,000 hadi 290,000 wakati ukiwa mkoani Mara utauziwa kwa Sh180,000.
Itakumbukwa Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya April 2023 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Machi 2022 ilikuwa Sh60,996 lakini ilipanda hadi Sh119,484 Machi mwaka huu.
Latest
