Chadema: Lissu amehamishiwa ukonga 

April 19, 2025 2:05 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya viongozi waandamizi wa chama hicho kukutana na uongozi wa Jeshi la Magereza. 

Dar es Salaam, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, amehamishiwa katika Gereza la Ukonga, kutoka katika Gereza la keko jijini Dar es Salaam alipokuwa awali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 19, 2025, na Msemaji wa chama hicho, Brenda Rupia viongozi waandamizi wa Chadema wamekutana mapema leo na uongozi wa Jeshi la Magereza na kufahamishwa kuhusu hatua hiyo.

“Chadema kinapenda kuuarifu umma kuwa mapema leo, tarehe 19 Aprili 2025, viongozi wakuu wa chama wamekutana na uongozi wa Jeshi la Magereza na kufahamishwa rasmi kuwa Mheshimiwa Tundu Lissu amehamishiwa katika Gereza la Ukonga,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya sintofahamu iliyotokea jana Aprili 18, baada ya viongozi na wanafamilia wa Tundu Lissu kutomkuta katika gereza la Keko walipoenda kutembelea.

Katika taarifa ya awali iliyotolewa Aprili 18, 2025, kupitia msemaji huyo huyo, chama kilieleza kuwa juhudi za kumtafuta Lissu katika Gereza la Keko hazikuzaa matunda, licha ya viongozi wa chama, mawakili wake, na wanafamilia kufika katika gereza hilo kwa nyakati tofauti.

“Viongozi wa chama akiwemo Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, mawakili, pamoja na wanafamilia wa Mheshimiwa Lissu walifika katika Gereza la Keko kwa nyakati tofauti ili kumuona mtuhumiwa huyo, lakini juhudi za kumwona hazikuzaa matunda baada ya kuelezwa kuwa hayupo katika gereza hilo, huku kukiwa hakuna taarifa yeyote juu ya mahali alipopelekwa,” ilieleza taarifa hiyo ya awali.

Hata hivyo, Chadema kupitia taarifa yake imetaarifu familia, wanachama wake na umma kwa ujumla kuwa sasa wanaweza kumtembelea Lissu kwa kufuata taratibu za kawaida za kumuona mahabusu katika Gereza la Ukonga.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, anatarajiwa kufika gerezani leo kwa ajili ya kumwona Lissu na kuzungumza naye.

Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi Aprili 9, 2025 alipokuwa katika mkutano wa kisiasa wa chama chake mkoani Ruvuma ambapo kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani humo Marco Chillya, mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa tuhuma za kufanya uchochezi wa kutofanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. 

Kwa mara ya kwanza Lissu alifikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Aprili 10, 2025 ambapo mpaka sasa bado anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama huku kesi yake ikiwa inaendelea kusikilizwa mahakamani na inatarajiwa kusikilizwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks