Kamati yaundwa kutathmini uchumi wa vyombo vya habari Tanzania
- Kamati hiyo itaangazia kwa undani hali ya uchumi katika vyombo vya habari na kutoa mapendekezo.
- Wadau wapongeza na kukosoa, wasema vyombo vya mtandaoni vimesahaulika.
Dar es Salaam. Huenda tasnia ya habari nchini Tanzania ikachukua sura mpya mara baada ya Serikali kuamua kulivalia njuga suala la uchumi wa vyombo vya habari pamoja na maslahi ya waandishi wa habari.
Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewaambia wanahabari leo Januari 24, 2023 kuwa ili kutimiza hilo, Serikali imeamua kuunda kamati ya kutathmini hali ya uchumi katika vyombo vya habari.
Uamuzi huo wa Serikali unakuja wakati ambao kumekuwepo na malalamiko mbalimbali ya waandishi wa habari kuwadai waajiri wao likiwemo tukio la hivi karibuni ambapo wafanyakazi wa Sahara Media walifanya mgomo ili kudai stahiki zao.
Miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo ambayo wanakamati wake sehemu kubwa ni wahabari ni pamoja na kupata taarifa ya hali ya vyombo vya habari kiuchumi na kiutendaji.
“Watafanya kazi ya kupata taarifa juu ya hali ya waandishi wa habari katila vyombo vya habari wakiwemo walioajiriwa, wenye mikataba, wawakilishi mikoani na wengine wanaoshirikiana na vyombo vya habari katika kupata habari, “ amesema Nape jijini Dar es Salaam.
Waziri Nape amesema kazi nyingine ya kamati hiyo ni kutathmini sababu ya changamoto za kiuchumi kwenye vyombo vya habari pamoja na kuja na mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo.
Soma zaidi
- Mwili wa Mtanzania aliyefia vitani Ukraine wasafirishwa kuja Tanzania
- Begi la umemejua: Mkombozi wa elimu Tanzania
Kamati hiyo itaongozwa na Tido Mhando, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Azam Media Group huku katibu akiwa Gerson Msigwa ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali ambae ataunda sekretarieti.
Wajumbe wengine wa kamati ni Dk Rose Ruben Mkurugenzi Mkuu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Mkurugenzi wa vituo vya ITV na Radio One, Joyce Mwavile, na Sebastian Maganga ambaye ni Mkuu wa Maudhui wa kampuni ya Clouds Media Group.
Katika orodha hiyo ya wajumbe yupo pia Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu, Kenneth Simbaya Mkurugenzi wa Shirikisho la Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UPTC) pamoja na Jackline Woison Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice Tanzania.
— Maelezo News (@maelezonews) January 24, 2023
Kwa mujibu wa Nape kamati hiyo itafanya kazi kwa muda usiozidi miezi mitatu na kuwasilisha taarifa ili zichukuliwe hatua nyingine.
Kuundwa kwa kamati hiyo kunakutokea wakati ambao wananchi na wanahahabari wanatarajia kusikia mabadiliko yaliyofanywa na Serikali katika Sheria ya Habari ambapo kwa mujibu wa Nape yapo katika hatua za mwisho.
“Nafurahi kutoa taarifa kwamba wizarani tumekamilisha utaratibu, na tumeshawasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye atayapeleka bungeni, “ amesema Nape.
Wadau wapongeza na kukosoa
Pamoja na hatua hiyo ambayo inatarajiwa kuleta matokeo chanya kwenye tasnia ya habari, baadhi ya wadau wamekosoa kitendo cha kamati kutokuwa na mjumbe hata mmoja kutoka vyombo vya habari vya mtandaoni.
Fredrick Bundala ambaye ni Mkurugenzi xwa televisheni ya mtandaoni ya Simulizi na Sauti, kupitia ukurasa wa Instagram ametoa maoni kwenye chapisho la Gerson Msigwa kuwa hatua hiyo ni kubwa lakini wasisahau kuangazia maslahi ya vyombo vya habari vya mtandaoni.
“Kubwa sana hii kaka, na kila la kheri katika kuyajenga. Naomba msisahau kuzungumzia online media. Bado, tunachukuliwa poa sana na makampuni. Kiuhalisia, wengi wetu tuna impact (matokeo), reach (ufikikaji) na influence (ushawishi) kubwa sana…., “ inasomeka sehemu ya maoni hayo
Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya michezo nchini Edo Kumwembe kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema uhalisia unafahamika Serikali ije na suluhu.
Latest