Mambo yatakayosaidia kukuza tasnia ya habari Tanzania

May 18, 2021 12:56 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na wanahabari kubadilika kutokana na mazingira.
  • Pia vyombo vya habari kukubali kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na uzalishaji wa habari bora.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha kuwa tasnia ya habari inakuwa endelevu na kuchangia katika maendeleo ya jamii, wadau wa tasnia hiyo wameshauri mambo mbalimbali ya kufanyia kazi ikiwemo kuboresha uzalishaji wa habari, kuongeza ubunifu na matumizi ya mifumo ya kidijitali. 

Mapendekezo hayo yametolewa leo Mei18, 2021) katika mdahalo maalum wa mtandaoni  uliondaliwa na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Afrika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya ya Wiki ya Ubunifu Tanzania (#IWTz2021). 

Mjadala huo ulibeba dhima ya “njia mbalimbali za kuzingatia katika ujenzi wa tasnia bunifu ya habari nchini Tanzania.”

Mkurugenzi  Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema zama zimebadilika na teknolojia imebadilika na hivyo vyombo vya habari na wanahabari wanahitaji wabadilike ili kuendana na mazingira ya sasa hasa katika kusambaza habari.  

Dausen ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika mjadala huo akiongelea amesema waandishi wa habari wanatakiwa kutengeneza maudhui au habari bora ambazo zimechakatwa kwa ubunifu mkubwa ili kufikia mahitaji ya walaji.

“Ni wakati wa kujifunza zaidi mabadiliko ya watu wanavyotumia habari ili kile tunachokifanya kiendane na kile watu wanachokitaka. Tasnia ya habari inabadilika kwa kasi sana, hivyo vyombo vya habari viende na kasi hiyo,” amesema Dausen

Dausen ambaye ni Mhariri Mkuu wa tovuti ya habari ya www.nukta.co.tz ameshauri wadau wa tasnia ya habari ikiwemo vyombo vya habari kuwekeza katika kutoa mafunzo kwa wanahabari ili kupata ujuzi ikiwemo wa mifumo ya kidijitali ya usambazaji habari, uthibitishaji habari na habari za takwimu. 

Mdahalo maalum wa mtandaoni uliondaliwa na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Afrika katika maadhimisho ya ya Wiki ya Ubunifu Tanzania. Picha| Gift Mijoe.

Sehemu kubwa ya watumiaji wa habari wako mtandaoni, hivyo kuna haja ya vyombo habari kuwafuata na kusoma tabia zao ili kuhakikisha wanaendelea kuendelea kuwepo katika soko la habari. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes, Kennedy Mmari ambaye amezungumzia mada ya kuhamia mtandaoni kama ni suluhu pekee ya kujiimarisha kibiashara katika tasnia ya habari, amesema kufanya hivyo siyo suluhu pekee kwa sababu tasnia hiyo inafanyika katika namna tofauti kulingana malengo ya kila chombo cha habari. 

Mmari ameshauri vyombo vya habari kuwekeza katika mifumo ya dijitali na kuangalia zaidi katika uwezo wa watumiaji wa simu wanavyoweza kuyafikia maudhui katika tovuti, programu tumishi za simu (Apps) na mitandao ya kijamii ya kampuni husika. 

“Tufikilie simu kwanza. Tufikirie ni kwa namna gani tumeyafanya maudhui yetu kuwa sambamba na watumiaji wa simu. Tunahitaji kufikika kwa urahisi kwa simu kwa sababu huko watu wengi ndiyo wanatumia maudhui ya habari,” amesema Mmari.

Ushirikia wa wadau mbalimbali

Mbali na kuongeza ubunifu na kuzalisha habari bora, kuna kina kila sababu za kuongeza ushirikiana kati ya taasisi zinazofundisha wanahabari na vyombo vya habari ili kuwa na ajenda ya pamoja kukabiliana na changamoto za ujuzi na maarifa yanayohitajika kwa sasa. 

Mkurungenzi Mtendaji wa kampuni ya habari ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu amesema upo umuhimu mkubwa kuunganisha kizazi kipya na watu wenye ujuzi waliopo kwenye tasnia ya habari kwa muda mrefu kuliko vijana. 

“Vyuo vikuu vinatakiwa vibadilike na viendane na mabadiliko haya yanayotokea kwenye tasnia ya habari. Kinachobadilika ni mifumo ya kuwasilisha habari,” amesema Machumu huku akilenga zaidi mitaala inayotolewa vyuoni.


Soma zaidi:


Wakati Bakari akishauri vyuo na vyombo habari kushikamana katika kuwafunza wanahabari bora, baadhi ya wadau wamependekeza kuwa sekta binafsi isiachwe pembeni ili kuhakikisha makundi yote kwenye jamii yanafikiwa kwa usahihi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media, Mike Mushi amesema ni wakati wa vyombo vya habari kutengeneza maudhui ya makundi ambayo hayafikiwi na vyombo vya habari vingi ikiwemo wakulima na mashirika mbalimbali zitakazoweza kuvutia uwekezaji na kuongeza mapato kwenye kampuni za habari. 

Amewataka wanahabari kubobea katika uandishi wa masuala na kujikita katika kuhudumia makundi mahususi kwenye jamii ambayo yatawanya kutokuyumbishwa na mabadiliko yanayotokea kwa sasa. 

Wiki ya ubunifu ni maadhimisho ya ubunifu ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka sita nchini Tanzania yanayolenga kuboresha hali ya ubunifu katika sekta mbalimbali zikiwemo mawasiliano, tasnia ya habari na sekta zingine.

Wiki Ya Ubunifu’ huwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili hatua zilizopigwa katika kuendeleza ubunifu nchini na maeneo yanahitaji msukumo wa kipekee wa matumizi ya teknolojia.

Enable Notifications OK No thanks