Serikali kupitia upya mikataba ya wanahabari Tanzania

May 3, 2024 11:49 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema lengo ni kuboresha maslahi ya wahabari nchini.
  • Teknolojia, akili bandia tishio kwa vyombo vya habari Tanzania.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza mchakato wa kupitia upya mikataba ya wanahabari ili kuboresha maslahi ya tasnia hiyo kutokana na uwepo wa malalamiko ya muda mrefu kuhusiana na maslahi duni kwa watumishi hao.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani leo Mei 3, 2024 mkoani Dodoma, amesema licha ya Serikali kuhamasisha ajira zitokanazo na sekta binafsi bado ipo haja ya kupitia upya mikataba hiyo ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

“Sisi mkakati wetu ni kuzalisha ajira kwa sekta binafsi, upande wa Serikali tulichokifanya ni kuzalisha vyombo vya habari binafsi…

…Leo tumepata ujumbe hapa kwamba tasnia hiii inahitaji kukaliwa kwa karibu tuone mifumo ya ajira zenu na mikataba inayotumika kati ya mwajiri na mwajiriwa,” amesema Majaliwa.

Awali rais wa Muungano wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo aliwaambia wahudhuriaji kuwa karibu asilimia 80 ya wanahabari hawana ajira na mikataba ya kudumu hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kumudu gharama za maisha ikiwemo za matibabu.

“Tunashindwa kumudu gharama za kiafya tunapozipata kwa sababu hatuna bima ya afya na tunaomba kupitia kwako mheshimiwa Waziri Mkuu utaratibu ule (kifurushi maalum kwa wanahabari)  urejeshwe na tupo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha jambo hili linafanyika,” amesema Nsokolo.

Kwa mujibu wa utafiti mpya wa maoni ya wanahabari Tanzania uliozinduliwa hivi karibuni na taasisi ya Twaweza, zaidi ya nusu ya wanahabari sawa na na asilimia 60 hawana ajira za kudumu hali inayowafanya kukosa huduma muhimu kama bima ya afya na pensheni.

Ripoti hiyo inafafanua zaidi kuwa asilimia 31 kati ya wanahabari 1,200 waliohojiwa katika utafiti huo hawana mikataba ya kudumu, huku nusu (asilimia 50) wakipata mikataba hiyo kwa wakati.


Nukta habari:Bajeti ya kilimo yapaa kwa miaka mitano mfululizo


Tishio kwa vyombo vya habari bado lipo

Waziri Majaliwa amewaambia wanahabari mabadiliko ya sayansi na teknolojia, pamoja na akili mnemba(AI) yanayoshika kasi siku za hivi karibuni ni miongoni mwa mambo yanayotishia tasnia hiyo.

“Hii inatokakana na  kuwa na maarifa madogo ya matumizi ya akili bandia  au akili mnemba hususan linapokuja suala la kuandika habari za mabadiliko ya tabia ya nchi, maafa na changamoto za mazingira,” ameongeza Majaliwa.

Wakati Waziri Mkuu akitaja AI kama tishio, Nuzulack Dausen mdau wa teknolojia na Mkurugenzi wa Kampuni ya Nukta Africa amesema AI inaweza kuwa fursa ikiwa vyombo vya habari vitajifunza kuitumia vizuri.

“Teknolojia hii ni nzuri na inarahisisha utendaji kazi kwa ufasaha, hivyo watu hawapaswi kuogopa matumizi ya AI,” alisema Dausen Oktoba, 2023 wakati akiwasilisha mada katika wiki ya Azaki iliyofanyika jijini Arusha.  

Aidha, Majaliwa amewataka wanahabari kuongeza uelewa wao katika kuripoti masuala mbalimbali hususani yanayohusu mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuepuka kutoa taarifa zitakazoleta taharuki kwa jamii.

Pia, amewataka wanahabari kuzingatia uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi na  kutoa mchango chanya kwa jamii, kinyume chake, tasnia ya habari inaweza kuwa chanzo cha kufifisha maendeleo na hata kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW